HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 26, 2021

GGM yaipatia VETA vifaa vya Sh. Mil 132 kwa ajili ya mafunzo


Na Mwandishi Wetu, Moshi

Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Geita (Geita Gold Mine - GGM) imeipatia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) vifaa vyenye thamani ya Shilingi za Kitanzania milioni 132 kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kilimanjaro (VETA Moshi).

Hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo imefanyika leo, tarehe 26 Oktoba 2021, katika Chuo cha VETA Moshi, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Stephen Kagaigai, alikuwa Mgeni Rasmi na amevipokea kwa niaba ya Serikali na kuvikabidhi kwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, kwa ajili ya usimamizi wa matumizi yake. Katika makabidhiano hayo, Kampuni ya GGM iliwakilishwa na Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo, Bw. Simon Shayo.

Vifaa hivyo vimelenga kuboresha mafunzo ya Uanagenzi yanayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya VETA na Umoja wa Wachimba Madini nchini (TCM) kupitia mradi wa Mafunzo Maalum ya Ufundi kwa ajili ya Sekta ya Madini, maarufu kwa jina la IMTT.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mh. Stephen Kagaigai, ameushukuru GGM kwa msaada huo wa vifaa na kueleza kuwa matumaini yake ni kuwa vifaa hivyo vitakwenda kuleta mabadiliko makubwa katika karakana za chuo cha VETA Moshi na kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo zaidi na kuhitimu wakiwa na ujuzi na umahiri wa viwango vya kimataifa. Aliwaomba wadau wengine wa Ufundi Stadi kuiga mfano huo wa GGM na kuunga mkono kwa vitendo juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini.

“Nitumie fursa hii pia kuwaomba wanachama wengine wa TCM kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, za kuzalisha mafundi stadi mahiri kwa ajili ya viwanda vyetu. Ufundi stadi ndio msingi mkubwa wa maendeleo ya viwanda. Kwa hiyo, tukiimarisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi tutaleta matokeo makubwa kiuchumi; na hili ni jukumu letu sote,” alisema.

Amewashauri VETA na TCM kueneza mpango huo wa mafunzo kwa njia ya uanagenzi kwenye vyuo vingine vya VETA na kuanzisha miradi mingine inayofanana na huo ili manufaa yaliyopatikana kupitia chuo cha VETA Moshi yaweze kuenea nchi nzima na kuwanufaisha vijana wengi zaidi.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Kampuni ya GGM, Bw. Simon Shayo, ameiomba Serikali kuhakikisha fedha za Tozo ya Uendelezaji Ujuzi (Skills Development Levy - SDL) inayopelekwa kwenye Ofisi Waziri Mkuu itumike zaidi kuboresha mafunzo ya ufundi stadi na mengine yanayofanana na hayo ili kupanua wigo wa uendelezaji ujuzi.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu alishukuru kampuni ya GGM kwa kuwa mfano wa kipekee katika kuthamini na kuchangia juhudi za uendelezaji ujuzi.

Amesema tangu kuanzishwa kwa mradi wa IMTT, kampuni za GGM na Bulyanhulu Gold Mine Limited zimekuwa mfano wa kuigwa kwa kujitoa kwa hali na mali katika kufadhili uanzishwaji na uendelezaji wa mradi huu.


“Kampuni hizi mbili ndizo zilizotoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa karakana, ununuzi wa mitambo na zana mbalimbali za mafunzo, pamoja na kugharimia mafunzo maalum ya walimu yaliyofanyika nchini Afrika ya Kusini. Hata baada ya mradi kuanza wao ndiyo wamekuwa kinara katika kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa uanagenzi waliosoma kupitia mradi huu,” amesema.

Naye Katibu Mtendaji wa TCM, Bw. Gerald Mturi, ameishauri Serikali kuanzisha chombo kinachofanana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambacho kitakuwa na majukumu ya kukusanya na kusimamia Tozo ya Uendelezaji Ujuzi (Skills Development Levy-SDL) na kuigawa kwenye taasisi mbalimbali kulingana na mahitaji halisi na kwa ajili ya matumizi sahihi.

No comments:

Post a Comment

Pages