HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 27, 2021

Waliochora tatoo kwenye titi hawafanyiwi kipimo cha Mammography

Msimamizi wa Huduma za Radiolojia kutoka Taasisi ya  Saratani Ocean Road ( ORCI), Stephen Mkoloma akielezea namna mashine ya Mammography inavyofanya kazi.

 

Na Asha Mwakyonde, Dar es Salaam

OKTOBA kila mwaka ni mwezi wa uhamasishaji wa saratani ya matiti ambapo ulimwenguni kote huhamasisha, lengo ni kusaidia kuongeza umakini na msaada wa elimu kwa wanawake uchunguzi wa mapema.

Pia kuimarisha upatikanaji wa matibabu mapema wa ugonjwa wa saratani. Katika kutimiza lengo hilo Taasisi ya Saratani Ocean (ORCI), inatumia mwezi huo kuweka Kampeni maalumu ya Uchunguzi wa awali wa Saratani ya Matiti.

Katika uchunguzi huo mashine ya Mammography ndio kipimo kinachotumika kuchunguza saratani ya awali kwa wanawake na wanaume.

Akizungumza na gazeti hili kutoka Taasisi hiyo Msimamizi wa Huduma za Radiolojia Stephen Mkoloma anasema katika mashine ya kisasa ya Mammography endapo dada  amechora Tatoo  kwenye titi ameweka kipini amefanya upasuaji wa Plastic Surgery hawawezi kumfanyia kipimo kwa sababu tatoo zina kemikali ambazo zitakwenda kuonekana picha itakayopigwa.

Mkoloma anasema kama kuna ugonjwa kwenye titi wataalamu hawawezi kuuona kutokana na kemikali zilizopo.

"Ni urembo lakini inapotokea mtu ana tatizo la afya Ina athari. Tunashauri  akina dada na akina kaka kufanya urembo wa asili utakaosaidia kupata huduma," anasema Mkoloma.

Pia anashauri akina dada hao kuacha kuweka urembo wowote kwenye matiti ili kuepuka kukosa huduma pale wanapostahili kuzipata

WANAOSTAHILI KIPIMO CHA MAMMOGRAPHY

Msimamizi huyo wa Radiolojia anafafanua  kuwa vipimo vua Mammography vinafanyika kwa akina mama wenye umri kuanzia  miaka 40 na kuendelea.

" Hawa ambao wapo chini  ya miaka 40 tunashauri wafanye kwanza Ultrasound ya matiti kabla ya kufanya kipimo cha Mammography," anasema Mkoloma.

Mkoloma anafafanua kuwa sababu  inayo sababisha   kuwashauri ni kuwalinda akina mama dhidi ya athari ndogo ndogo ambazo zinaweza kutokea.

Anaeleza kuwa binti anapokuwa umri wa kuzaa seli zake zina uwezo mkubwa wa kutunza mionzi kwenye titi ndio maana wanashauri ili asiweze kupata madhara.

" Kama kipimo cha Ultrasound kitaonesha tatizo ambalo linahitaji kuthibitishwa na kipimo cha Mammography ndio aende kufanya kipimo hicho," anasema.

WANAUME

Anasema kwa upande wa wanaume wanaweza kufanya uchunguzi wakati wowote bila kuathitika kwa kuwa hawatumii matiti  kwa namna yoyote ile.

Mkoloma anaeleza kuwa dada ambaye atakuja kujifungua au kushika ujauzito matiti yake atatumia kwa ajili ya kunyobyesha.

" Kama seli zake zimepata athari ya mionzi inaweza kuathiri kwenye  unyonyeshaji wake," anasema Mkoloma.

Anasema kwa wanaume haina athari kwahiyo wakati wowote  anaweza kufanya kipimo cha Mammography bila kuangalia umri.

No comments:

Post a Comment

Pages