Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akifyeka moja ya shamba la mikorosho lililopo mlandizi Wilayani Kibaha ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa kampeni kimkoa kwa ajili ya kufyeka.
Na Victor Masangu, Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka wakulima wa zao la korosho kuweka mipango madhubuti ya kuhakikisha kwamba wanafyeka na kuyasafisha mashamba yao ili yawe masafi katika kipindi chote ili kuweza kutimiza malengo waliyojiwekea ya kupata korosho ambazo zina ubora unaotakiwa.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa halfa ya siku ya upandaji wa miti Kimkoa sambamba na ufyekaji wa nyasi katika mashamba ya korosho ambayo imefanyika katika eneo la mlandizi Wilayani Kibaha na kuhudhuliwa na viongozi mbali mbali wa serikali wakiwemo wakulima pamoja na viongozi wa vyama vya ushirika.
Kunenge alisema kwamba wakulima wa zao la korosho wanapswa kuhakikisha kwamba wanazingatia maelekezo yote ambayo wanapatiwa na wataalamu wa kilimo ili kuweza kilimo amabcho kina tija na kuleta faida hivyo amewataka kuweka mipango madhubuti ambayo itaweza kuwasaidia katika kujipatia kipato kupitia zao hilo la korosho.
“Kitu kikubwa hapa katika Mkoa wetu bado tuna maeneo mengi sana kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha mazao mbali mbali lakini mimi kitu kikubwa nawaomba katika hili mnatakiwa kulima kilimo chenye tija na sio kilomo amabcho hakina faida kwa kuwa mnatumia muda mwingi katika kuandaa mashamba yetu hivyo mwisho wa siku mnatakiwa kukifanya kilimo hiki kiwe cha biashara zaidi ili muweze kujiingizia kipato,”alisema Kunenge.
Aidha alisema kwamba serikali ya Mkoa wa Pwani katika kuimarisha kilimo cha mazao mbali mbali itaendelea kushirikiana bega kwa began a wakulima kwa lengo la kuweza kuwasaidia katika mambo mbali mbali ikiwemo suala la changamoto zinazowakabili katika madawa ya kupulizia wadudu, pamoja na mahitaji mengine ya pembejeo ambazo zitaweza kuwasaidia katika kuleta mabadiliko chanya ya kilimo.
“Mimi kama Mkuu wa Mkoa siwezi kuwaangusha wakulima na kwamba kipaumbele changu kikubwa ni katika zao la korosho, ufuta pamoja na mazao mengine na nitahakikisha ninayafutilia kwa ukaribu zaidi kwani ndio yataweza kusaidia kuboresha maisha ya wananchi wetu katika suala zima la kuwaongezea kipato na kukuza uchumi wao,”alisema Kunenge.
Akizungumzia kuhusiana na suala la upandajiwa wa miti alifafanua kuwa katika msimu huu wa mwaka 2021 hadi 2022 juma la miche ipatayo 8,288,007 ambayo ni sawa na asilimia 61.39 ya lengo la upandaji wa miti kimkoa ipo tayari kwa ajili ya kuweza kupandwa ambapo kati hiyo miche 504,000 imezalishwa katika kitaru cha Mkoa.
Kadhalika alisema kwamba shughuli mbali mbali za binadamu zinazofanywa katika misitu ikiwemo ukataji wa miti ovyo, fito, nguzo za ujenzi, uchomaji wa mkaa, uchimbaji wa mchaja pamoja na upasuaji wa mbao vinachangia kwa kiasi kikubwa kupotea kwa uoto wa asili.
“Madhara makubwa ambayo yanatokana na ukataji wa miti ovyo kunatajwa na wataalamu wa mazingira ni kusababisha kupungua kwa maji safi, na kuongezeka kwa wa magonjwa ya wanyama na mimea, kutoweka kwa baadhi ya aina za wanyama na mimea hivyo nawaasa inatakiwa tutunze na mazingira yetu na kupanda miti,”alibainisha Kunenge.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sarah Msafiri alisema kwamba katika zoezi hilo wamefanikiwa kupanda zaidi ya miti ipatayo 504 na kuwahiza wananchi kuhakikisha wanaitunza na kuilinda ili iweze kudumu kwa kipindi cha muda mrefu na kuongeza kwamba kuna haja ya viongozi kwenda mashambani kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kwa kusikiliza changamoto zao.
Naye Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika mkoani pwani CORECU Mussa Ngeresa alibainisha kwamba lengo lake kubwa ni kuendelea kuwasaidia wakulima katika halmashauri zote kwa kuwasikiliza changamoto mbali mbali ambazo zinawakabili ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi pamoja na kuwawezesha wakulima suala la viatilifu kwa mashamba ambayo yameendelezwa.
Mkurugenzi mkuu wa bodi yak korosho Tanzania Francis Afred alisema kwamba kwa sasa wameweka mikakati madhubuti kwa ajili ya kuongeza zaidi kasi ya uzalishaji wa zao hilo kutoka wastani wa tani laki tano hadi kufikia tani laki 7 kwa kipindi cha mwaka 2025 hadi 2026 lengo ikiwa ni kuwaboreshea mazingira mazuri wakulima hao.
No comments:
Post a Comment