HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 25, 2022

MAJALIWA: PANUENI WIGO WA MATUMIZI YA GESI ASILIA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Nishati kuendelea kupanua wigo wa matumizi ya nishati ya gesi asilia ili kupunguza athari za kimazingira zinazotokana na ukataji wa misitu nchini.

 

Amesema hayo leo (Jumatano, Mei 25, 2022) wakati alipotembelea maonesho ya Majukumu ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

 

Amesema kuwa Wizara kwa sasa iendelee kupanua wigo wa kufikia Watanzania wengi zaidi katika mikoa mbalimbali nchini. “Tupanue wigo na huduma hii iwafikie watu, tumeanza na Dar es Salaam, tuje kwenye majiji, manispaa zetu na hata hapa Dodoma tuwe na tawi na kazi hii iendelee”

 

Aidha, Waziri Mkuu amewataka watendaji wote katika sekta ya nishati kuhakikisha wanasimamia upatikanaji wa nishati ya umeme na nishati nyingine ikiwemo mafuta ili kuendelea kuiwezesha nchi kupata fursa ya kuendelea kukua kiuchumi.

 

“Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imeitaka Serikali kuhakikisha upatikanaji wa umeme katika vyanzo vyetu unaimarishwa, kuendelezwa na kuhakikisha usambazaji wa umeme unawafikia wananchi mpaka vijijini ili kila Mtanzania anufaike kwa kupata nishati hiyo”

 

Maonesho hayo ya siku tatu yaliyoanza Mei 23, 2022 katika viwanja vya bunge yalikuwa na lengo la kuwawezesha Waheshimiwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuuliza maswali kuhusu huduma zinazotolewa na Wizara ya Nishati na taasisi zake.

 

No comments:

Post a Comment

Pages