HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 28, 2022

Vijana wakumbushwa kuchangamkia fursa mikopo ya serikali


Na Mwandishi Wetu, Tanga


VIJANA wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga, wameshauriwa kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba inayotolewa na halmashauri zote nchini.

Rai hiyo imetolewa leo Mei 28,2022 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Sahili Geraruma wakati akikagua shughuli za Kikundi cha Uvuvi cha Vijana cha Neymar, katika Kijiji cha Mongavyero Kata ya Kwale wilayani Mkinga.

Akizungumza baada ya kukagua mradi wa kikundi hicho Geraruma amewapongeza vijana hao kutokana kwa kutumia mkopo waliopewa vizuri kujiajiri na kutengeneza ajira zaidi ya 100.

"Nawapongeza kwa sababu moja tu; kujituma na kufanya marejesho kwa wakati. Kwa sababu mngeweza kukaa vijiweni mkajiingiza katika makundi mabaya mkashawishika kufanya vitendo viovu.

"Nawasihi vijana wenzangu mchangamkie fursa hii ya mikopo inayotokana na mapato ya ndani ya serikali inayotolewa na halmashauri zote nchini ambapo mnajiunga kwenye vikundi wanawake wanapata asilimia nne, vijana nne na wenzetu wenye ulemavu asilimia mbili tena mikopo hii haina riba," amesema Geraruma.

Awali, akisoma taarifa ya kikundi Mwenyekiti wa kikundi hicho, Amiri Maamuni alisema kikundi chao kilianzishwa mwaka 2020 na kina wanachama saba ambao wote wanafanya shughuli za uvuvi.

"Malengo ya kikundi chetu ni kufanya kazi kwa bidii ili kujikwamua kiuchumi na kuo ngeza ajira kwa vijana wengine. Kikundi kinafanya shughuli zake kwa pamoja chini ya Ofisa Maendeleo aliyeko kata husika, aidha hadi sasa kikundi kimezalisha ndoo za dagaa 30 zenye thamani ya Sh milioni 1.47," amesema.

Mwenyekiti huyo amesema gharama za mradi wote ikiwamo kutengeneza chombo cha uvuvi na vifaa vya kuvulia ni Sh milioni 17 walizokopeshwa na halmashauri.

Ukiwa wilayani Mkinga, mwenge umezindua na kukagua miradi mingine saba ikiwamo mradi wa maji uliopo Kijiji cha Manza unaotokana na michango ya mwenge, madarasa mawili na ofisi moja ya walimu katika Shule ya Sekondari Zingibari, mradi wa kisima cha maji cha Maforoni na kupokea taarifa ya utekelezaji wa zoezi la anuani za makazi na uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika nchini Agosti 23, mwaka huu.

Aidha, mwenge pia umezindua na kuweka jiwe la msingi katika Zahanati ya Mavovo na kutoa ujumbe wa mwenge, kufungua kituo cha mafuta (petrol station) Maramba, ujenzi wa daraja la Kauzeni, ujenzi wa Barabara ya Mapatano-Mbuyuni inayojengwa kwa kiwango cha changarawe.

Pamoja na mambo mengine, katika mkesha wa mwenge katika Viwanja vya CCM Maramba, ilifanyika vipimo mbalimbali vya kiafya ambapo ilitolewa chanjo ya Uviko 19, upimaji wa Virusi Vya Ukimwi (VVU) na uchangiaji wa damu.

Akisoma taarifa ya saa 24 zilizopita mwenge wa uhuru, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Kanali Maulidi Surumbu amesema ulihamasisha upimaji wa VVU kwa hiari ambapo jumla ya watu 562 walipimwa ambapo kati yao wanaume walikuwa 252 na wanawake 91.

"Kati ya hao waliopimwa watu wanne walikutwa na maambukizi ambapo wanaume walikuwa watatu na mwanamke mmoja na huduma ya ushauri nasaha ilifanyika na wote wanne walikubali kuanza matibabu ya dawa za kufubaza VVU.

"Waliochanja chanjo ya Uviko 19 walikuwa 554, wanaume 229 na wanawake 325 huku waliochangia damu walikuwa 40, wanaume 39 na mwanamke mmoja na kiasi kilichopatikana ni chupa 40 sawa na asilimia 80," amesema.

Mwenge wa Uhuru leo utakuwa wilayani Muheza ambapo pamoja na mambo mengine utakagua na kuzindua miradi minane yenye thamani ya Sh bilioni 1.7.

No comments:

Post a Comment

Pages