HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 28, 2022

WATU wenye ulemavu waiomba serikali kuwawezesha kupata elimu

 

Jackiline Fabian mama mwenye ulemavu wa viungo akiwa katika eneo la mradi wake wa ufugaji wa mbuzi wa maziwa.

 

Na Lydia Lugakila, Kagera

Watu wenye ulemavu wa viungo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wameiomba serikali mkoani humo kuwawezesha kupata elimu kuhusu miradi midogo midogo itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi.

Wakizungumza na mtandao huu wakazi hao waishio kata ya Kahororo manispaa ya Bukoba akiwemo Mwalimu Jackiline Fabian na Mwalimu Deusdedith Petro wameipongeza serikali kwa namna inavyopambana kuhakikisha inaweka miundo mbinu rafiki kwa watu wenye ulemavu ikiwemo kuwatambua katika  huduma za afya, shule na upande wa vifaa saidizi ambapo wamesema kuwa bado wanakumbana na changamoto ya kutokuwepo elimu kuhusu miradi midogo inayoweza kuwanufaika na kuondokana na kubebwa au kusubiri kupewa.

Bi Jackiline ambaye ni mwenyekiti wa Shivyawata wilaya ya Bukoba na ni mama wa watoto 4 anasema kuwa licha ya kuwa mtu mwenye ulemavu wa viungo tangu akiwa na umri wa miaka 3 sasa ana umri wa miaka 35 tayari ameikubali hali hiyo na kujikita zaidi katika miradi midogo midogo ikiwemo ufugaji wa mbuzi wa maziwa, sungura ,kuku na bustani ya mboga mboga jambo lililomsaidia kutunza familia yake huku akiiomba serikali kusaidia kutoa elimu juu ya miradi midogo midogo ili kundi hilo liihudumie ipasavyo na kujinufaisha kiuchumi kuliko kusubiri kupewa.

"Licha ya kuwa mtu mwenye ulemavu wa viungo nashukuru mwenyezi Mungu bado nazidi pambana nikiwa na imani na serikali yangu kwani imetambua kundi hili niombe pia itujali zaidi kwa kuweka miundombinu rafiki  ikiwemo mazingira ya shule kwa watoto wetu hasa ya ngazi kwa ajili ya kuingia kwenye vyumba vya madarasa, vyoo alisema Bi Jackiline.

Aidha ameiomba jamii kutowaficha watoto wenye ulemavu majumbani kwani wanawakosesha mahitaji yao ya msingi ikiwa ni pamoja na elimu na kuwa kwa kufanya hivyo wanakwamisha juhudi za serikali pale wanapokuwa wakifanya utambuzi au takwimu mbali mbali.

Ameongeza" niiombe serikali kuielimisha jamii juu ya kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika masula ya kisiasa lengo likiwa ni kuijenga Tanzania moja ambapo pia natarajia kuwa mwanasiasa mkubwa hii ni ndoto yangu ya muda mrefu" alisema Bi Jackiline.

Naye Mwl Deusdedith Petro amesema kuwa endapo mtu mwenye ulemavu akijengewa mazingira mazuri ataepuka kusubiri kupewa, hivyo amewahimiza wadau mbali mbali kusaidiana na serikali ili kuwaibua watoto wenye ulemavu ili wapelekwe shule kukamilisha ndoto zao za baadae.

Hata hivyo kwa upande wake katibu wa chama cha wasioona Kagera amefurahishwa na namna ambavyo watu wenye ulemavu wanavyojishughulisha katika kujipatia kipato huku akiiomba serikali kuweka takwimu, nzuri ili kuwatambua na kujua wana uhitaji gani.

No comments:

Post a Comment

Pages