Na Mbaraka Kambona, Geita
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema Serikali ipo kwenye
mchakato wa kushirikisha wadau wa sekta ya mifugo kupanga bei elekezi za
kuuzia mifugo katika minada ili kuwawezesha wafugaji na
wafanyabiashara kuuza mifugo yao kwa bei ambayo wao watakuwa wameshiriki
kuipanga.
Alitoa kauli
hiyo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnada wa
Kimataifa wa Buzirayombo unaojengwa Wilayani Chato, Mkoani Geita
Mwishoni mwa wiki.
Alisema
suala la kuwa na bei elekezi, Serikali inalifanyia kazi na tayari
Wataalam walishaandaa na hatua iliyopo sasa ni ya kuwashirikisha
wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo ili kwa pamoja waweze kukubaliana
na kuja na bei ambayo itakuwa imeridhiwa na pande zote.
"Bei
elekezi ikitoka ndio itakuwa mahali pa kuanzia na kwenda juu, hivyo
tunalifanyia kazi suala hilo na muda sio mrefu tutato muelekeo wa jambo
hilo", alisema
Aliongeza
kwa kusema kuwa sambamba na bei elekezi Serikali inataka sasa mifugo
yote nchini ianze kupimwa kwa kilo kama ambavyo mifugo itapimwa kwa kilo
katika mnada huo wa kisasa wa Buzirayombo.
"Minada
yetu yote tutakayoizindua safari hii tunataka iwe na mizani ya kupimia
uzito wa mifugo na hili tunataka lifanyike pia katika minada yote ya
awali inayomilikiwa na Halmashauri zetu hapa nchi ili tuondokane na
vitendo vya kuwapunja wafugaji wetu", aliongeza
Kwa
upande wake, Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe. Medard Kalemani aliishukuru
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kujenga mnada huo wa
kimataifa Wilayani humo huku akiongeza kwa kuiomba kuhakikisha mradi
huo unamalizika haraka ili wananchi wa Kanda ya Ziwa na maeneo mengine
waanze kuona matunda yake.
No comments:
Post a Comment