Na WMJJWM, Dodoma
Wakurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara na Taasisi wametakiwa kuhakikisha Masuala ya Jinsia yanapewa kipaumbele na kuingizwa kwenye Bajeti, Sera na miradi yote ya maendeleo kwa kuwa na ushiriki sawa kati ya Wanawake na Wanaume.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati akifungua kikao kazi cha kupitia andiko la hali ya Jinsia Tanzania Bara kilichofanyika Jijini Dodoma tarehe 27 Septemba, 2022.
Waziri Gwajima amewataka pia Maafisa wa madawati ya Jinsia kwenye Wizara na Taasisi kuwasilisha taarifa ya kila baada ya miezi mitatu kuhusu utekelezaji wa bajeti inayozingatia masuala ya Jinsia katika uhalisia wake kwenye Wizara yenye dhamana na masuala ya Jinsia.
"Uwepo wa usawa wa Kijinsia katika nyanja zote utasaidia kuweka uhalali wa mipango inayohusu masuala ya kiuchumi, na masuala yanayohusu Sekta ya Elimu hasa katika ushiriki sawa kwenye masomo ya (Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM)), vilevile, ushiriki sawa katika uongozi na katika ngazi za maamuzi na usawa katika masuala ya Afya bora, Kilimo na sekta zingine zote" amesema Mhe. Gwajima.
"Tunatakiwa wote tufahamu kuwa, ajenda ya jukwaa la kizazi chenye usawa na mahsusi uwezeshaji wanawake kiuchumi, utekelezaji wake uko kwenye Wizara na sekta zote pamoja na taasisi zake" ameongeza Mhe. Gwajima.
Mhe. Gwajima amesema katika kutekeleza Ajenda ya Jukwaa la kizazi chenye usawa iliyotolewa na Mhe. Rais Samia nchini Ufaransa mwaka 2021, jitihada zimefanyika ikiwemo kuzindua mwongozo wa uanzishwaji na uendeshaji wa Majukwaa ya Wanawake kiuchumi.
Akizungumza kabla ya ufunguzi wa kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amewataka washiriki wa kikao hicho kutoa maoni na michango yao itakayoliboresha andiko hilo kwa sababu kitakuwa ndiyo nyenzo muhimu ya utendaji wao katika Masuala ya uwezeshaji Wanawake kiuchumi.
"Kikao kazi hiki pamoja na kuwa kinaklenga kutoa maoni na michango lakini tunaamini kitatumika kama Jukwaa la watu kujifunza na kupata uzoefu na hatimaye kutupa mawazo yatakayoakisiwa kwenye rasimu hii ili nyaraka hii ije kuwa na umiliki wa kila mmoja" amesema Mpanju
Kwa upande wake Mwakilishi wa UNWOMEN Tanzania Usun Mallya amebainisha kwamba, andiko hilo ni nyenzo muhimu ya kupima utekelezaji wa maazimio ya kikanda na Kimataifa kwa nchi wanachama za umoja wa Mataifa.
"Andiko hili upimaji wa utekelezaji unatumia viashiria ambavyo vipo katika matamko na makubaliano ya Kimataifa na kikanda yanayohusu usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa Wanawake" amesema Usu.
Naye mmoja wa washiriki wa kikao kazi hicho Oscar Kashaigili kutoka Wizara ya Nishati amesema maelekezo yaliyotolewa na Waziri yameelekea kwa wahusika sahihi kwani ndiyo wanasimamia Mipango na fedha za Taasisi.
Andiko linalojadiliwa katika kikao kazi hicho limeandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa UNWOMEN na limejikita kwenye maeneo takribani 14 kupima uwiano wa kijinsia.
No comments:
Post a Comment