HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 22, 2022

Bodi Mpya NCC yazinduliwa, yatakiwa kutekeleza majukumu kwa kufuata sheria, taratibu na weledi wa utumishi wa umma


 
Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Bodi ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) imetakiwa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, taratibu, weledi na maadili ya utumishi wa umma.

Aidha, imetakiwa kutoa miongozo ya thamani halisi ya miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara ili kuokoa fedha za Serikali zinazopotea kutokana na kukosa miongozo sahihi.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi- Sekta ya Uchukuzi Atupele Mwakibete wakati akizindua Bodi Mpya katika Ofisi za Wakala wa Majengo Nchini (TBA) zilizopo jijijni humo.

Amesema kuwa kutokana na kukosa miongozo sahihi ya gharama  halisi ya miradi ya maendeleo Serikali imekuwa ikipata kilio cha kuingia gharama tofauti na awali hivyo ameitaka bodi hiyo kuhakikishia inaondoa changamoto hiyo.

" Bodi ina jukumu la kuhakikisha thamani ya miradi ya maendeleo inabaki ileile hii itawezekana mkitekeleza majukumu yenu kwa kufuata na kuweka mwongozo sahihi wa ujenzi," amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete ameitaka bodi hiyo kutekekeza majukumu yake kikamilifu ikiwemo kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya hiyo pamoja na kuyafanyia kazi mabadiliko yote yaliyoanzishwa.

Ameongeza kuwa ana imani kubwa bodi hiyo itatekeleza majukumu yake kwani wajumbe wake wameshapatiwa mafunzo ya utekelezaji na kuikumbusha kuepuka vitendo vya rushwa na udanganyifu.

Amemuagiza Naibu Katibu Mkuu Ujenzi kuyasimamia, kuyaratibu na kuyafanyia kazi mabadiliko atakayoletewa kwa haraka iwezekanavyo ili yaweze kuleta tija iliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Baraza hilo,  Dkt Matiko Mturi  ameyataja majukumu yake kuwa ni pamoja na kuwezesha maendeleo ya kukua kwa sekta ya ujenzi nchini.

Dkt Mturi ameeleza kuwa jukumu lingine ni kufanya utafiti na kuratibu kufanyika kwa utafiti
utakawezesha maendeleo katika sekta ya ujenzi lakini pia kuwezesha migogoro inayotokea katika sekta ya ujenzi hasa kwenye miradi ya ujenzi kupata utatuzi wa haraka na kuleta tija.

‘Pamoja na kuwa na mafanikio tumekuwa na changamoto chache ikiwemo ya uhaba wa wataalamu wa kada za uhandisi,za ukadiriaji majenzi na kada za ubunifu majengo.

Nae, Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) Dkt Fatma Mohamed amemuahidi Naibu Waziri kuwa watafanya kazi kwa bidii na ueledi ili kutimiza majukumu yao ipasavyo ili kuleta mabadiliko katika sekta ya ujenzi nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages