Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB,) imeshauriwa kuendelea kutoa huduma kwa wateja wao kupitia ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam inayohudumia na maeneo yanayozunguka licha ya kuhamia rasmi makao makuu ya Nchi Dodoma tangu Septemba 30, 2022 ili kuweza kuwafikia watanzania wengi zaidi kwa wakati.
Hayo
yameelezwa jijini humo na Kamishna wa Sera wa Bodi ya Wataalamu wa
Ununuzi na Ugavi (PSPTB,) Fredrick Mwakibinga katika mahafali ya 11 ya
Wahitimu wa Mitihani ya Kitaaluma ya PSPTB alipomwakilisha Katibu Mkuu
wa Wizara ya Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba.
"Napenda
kuwapongeza wahitimu wote ambao mtatunukiwa vyeti pamoja na shahada za
umahiri ila mfahamu kazi kubwa mnayokwenda kuifanya kwa jamii....
Ninaelewa vizuri hatua na changamoto mlizopitia leo mnastahili
pongezi....Jitihada zinazofanywa na bodi zinaonekana dhahiri endeleeni
kuwahudumia watanzania katika ofisi za hapa Dar es Salaam na Dodoma pia "
Amesema Mwakibinga.
Pia
Mwakibinga amewapongeza na kuwashukuru wahitimu hao kwa uvumilivu wa
kusubiri kuteuliwa kwa bodi ya wakurugenzi na kueleza kuwa Wizara
inatambua changamoto iliyojitokeza na tayari imechukua hatua ili
changamoto hiyo isijitokeze tena wakati mwingine.
Aidha
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PSPTB Jacob Kibona amesema mahafali
hiyo ni ya 11 tangu kuanzishwa kwa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi
2007 na kueleza kuwa kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Bodi hiyo,
matokeo yote ya mitihani ya kitaaluma ya PSPTB ni lazima yapitiwe na
kuidhinishwa na bodi ya Wakurugenzi.
"Kwa
bahati mbaya kuanzia septemba 2019 hadi novemba 2021 PSPTB haikuwa na
bodi ya wakurugenzi baada ya iliyokuwepo awali kumaliza muda wake hali
hii ilipelekea kutokufanyika kwa mahafali kwa miaka mitatu napenda
kuchukua nafasi hii kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha na
Mipango hatimaye bodi ya wakurugenzi imeteuliwa Novemba 2021." amesema
Kibona.
Mkurugenzi
Mtendaji wa PSPTB, Godfred Mbanyi amewaasa na kuwataka wahitimu hao
kufanya kazi kwa kufata maadili ya kitaaluma ili kulinda heshima ya fani
hiyo na kuleta ufanisi katika matumizi ya rasirimali za Umma kwa
manufaa ya Taifa .
"Tunaposema
maslahi aidha mkitumika sekta binafsi au sekta za Umma wote mnahitaji
kufanya kazi kwa maadili, Tunahitaji kampuni binafsi zikue kwa kufanya
biashara kubwa ili ziweze kulipa kodi na Nchi iweze kuendeleza shughuli
za maendeleo katika jamii." Amesema Mbanyi.
No comments:
Post a Comment