Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) wameadhimisha Kilele cha Wiki ya Usalama wa Reli yaliyofanyka leo Kamata jijini Dar es Salaam.
Aidha, Wiki ya Usalama wa reli huadhimishwa tarehe 10 hadi 13 mwezi Oktoba kila mwaka kwa Wanachama wa Vyama vya Reli Kusini mwa Afrika (SARA) ikiwa na lengo la kuendelea kusisitiza na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usalama wa reli.
Mwaka huu Tanzania imekuwa mwenyeji ambapo maadhimisho hayo yamebba kauli mbiu isemayo “CHUKUA TAHADHARI, TRENI ZINA MWENDO WA HARAKA, NI HATARI”.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua vyema umuhimu wa ulinzi na usalama wa miuondombinu ya reli ndiyo maana inaendelea kutoa fedha kujenga na kuboresha miundombinu ya reli.
Naibu Waziri Mwakibete ametoa wito kwa wafanyakazi wa TRC na Taasisi zingine wajiendeleze kwa kutoa mafunzo ili kuwapa ujuzi watumishi, “nilivyokua napita kwenye mabanda nimeona TRC na LATRA wamepeleka vijana wao nje kupata elimu na ujuzi mpya kwa hiyo na taasisi zingine ziige taasisi hizi ili kuweza kuendesha na kusimamia miradi mikubwa kama SGR’’ amesema Mhe. Atupele.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa LATRA, CPA Habibu Suluo amesema LATRA na TRC ni washirika wa SADC, katika siku hii ya kilele cha wiki ya usalama wa reli ametoa wito kwa watumiaji wa reli wakiwemo wananchi na wadau kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri katika kulinda miundombinu ya reli vilevile watumishi kufanya kazi kwa weredi katika kuzingatia Sheria za kazi za reli ikiwemo kuhakikisha usalama wa behewa, vichwa vya treni kabla havijaanza safari na vikiwa safarini.
Nae, Mkurugenzi Mkuu TAZARA Mhandisi, Bruno Ching’andu amesema kuwa kila mtu afikirie kuhusu usalama wake na wenzake kwa kutumia elimu inayotolewa kwani inasikitisha kuona kwamba kila mwaka zaidi ya watu 35 barani Afrika wanapoteza maisha kutokana na ajali ndogo za treni inayotokana na uelewa mdogo wa jamii kuhusu usalama wa reli.
“Watu hawajali kabisa kuhusu ulinzi na usalama wao, hawajishughulishi wala kuchukua tahadhari, wanaamini treni inawaona na itasimama, hii ina sikitisha sana, kila mwaka zaidi ya watu 35 Afrika wanapoteza maisha kutokana na ajali ndogo za treni, hii ni hatari inabidi jamii ieleweshwe na kupewa elimu ya masuala ya usalama” amesema Eng. Bruno Ching’andu.
Mkurugenzi Mkuu TRC, Masanja Kadogosa amewashukuru wananchi, wafanyakazi wa TRC na umma kwa ujumla kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika jitihada zinazofanywa kuhakikisha miundombinu ya reli inakuwa salama.
Mkurugenzi Mkuu TRC, aliongeza kuwa “Katika kuadhimisha wiki hii wananchi wameonesha ushirikiano mkubwa kwa kujitokeza kwa wingi katika mikutano iliyoandaliwa kwa ajili ya kutoa elimu ya uelewa kuhusu usalama wa reli. Niwasihi waendelee kuwa mabalozi kwa kuwapatia elimu hiyo wananchi wengine”.
No comments:
Post a Comment