Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb)
(katikati), akiongoza kikao cha Kundi la Kwanza la Kanda ya Afrika
(Africa Group 1 Constituency) katika Shirika la Fedha la Kimataifa
(IMF), linalojumuisha Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka
nchi 23 za Afrika, kilichofanyika Makao Makuu ya Shirika hilo, wakati wa
mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kmataifa
(IMF), inayoendelea Jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Na Benny Mwaipaja, Washington DC
TANZANIA
imemaliza muda wake wa miaka miwili wa kuwa Mwenyekiti wa Kundi la
Kwanza la Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency) katika Shirika
la Fedha la Kimataifa (IMF), linalojumuisha Mawaziri wa Fedha na
Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi 23 za Afrika, ambapo katika muhula
wake, mafanikio makubwa yamepatikana, licha ya kukabiliwa na changamoto
za UVIKO-19 na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema
hayo Jijini Washington D.C, nchini Marekani, baada ya kuongoza mkutano
wake wa mwisho Mawaziri na Mgavana wa Kundi hilo na kukabidhi rasmi
uongozi wa miaka mingine miwili kwa Namibia kama Mwenyekiti na nchi ya
Botswana kama Makamu Mwenyekiti.
Katika
kipindi cha uongozi wa Tanzania, Kundi hilo limenufaika kwa ongezeko la
upatikanaji wa rasilimali fedha kwa nchi wanachama wake na kuwa na
sauti zaidi katika shughuli za uendeshaji za Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF).
Nafasi
ya Tanzania katika kundi hilo iliwezesha kuimarisha mashirikiano kati
yake na IMF ambapo imeshudiwa Shirika hilo likiongeza uwekezaji wake
nchini kwa takriban shilingi trilioni 1.3. zilizotolewa kama mkopo usio
na riba kwa ajili ya kukabiliana na athari za UVIKO-19 katika sekta za
elimu, afya, maji na utalii hivi karibuni.
Aidha,
katika kipindi hicho, IMF iliidhinishia Tanzania mkopo nafuu wenye
thamani ya jumla ya shilingi trilioni 2.7 za kukabiliana na athari za
UVIKO-19 na vita ya Ukraine ambapo tayari kiasi cha shilingi bilioni 347
zimeshatolewa ili kuleta ahueni kwa wanachi kupitia utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Alisema
kuwa ajenda kubwa ya mkutano huo ambao aliuongoza kwa mara ya mwisho,
ilijikita katika kutafuta namna IMF inavyoweza kuzisaidia nchi wanachama
kukabiliana na uhaba wa chakula na mfumuko wa bei uliosababishwa na
athari za UVIKO-19, vita vya Urusi na Ukraine na mabadiliko ya tabia
nchi.
Dkt.
Nchemba alilita Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuendelea
kushirikiana na uongozi mpya wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki
Kuu kutoka Kundi la Kwanza la nchi za Afrka, kwa kutoa mikopo na misaada
itakayosaidia kufufua uchumi na kukabiliana na uhaba wa chakula katika
nchi hizo.
Aidha,
Dkt. Nchemba, alitoa wito kwa nchi wanachama wa Kundi hilo kuwa na
sauti moja ya kupigania maslahi ya nchi zao katika Shirika hilo kubwa la
Fedha la Kimataifa na kuhakikisha wanatunga sera rafiki
zitakazoimarisha sekta za uzalishaji, hususan kwenye kilimo.
No comments:
Post a Comment