HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 23, 2022

WATANI MTUMWA HANA MBAMBAMBA




Na John Richard Marwa

Watani, eeeh!, 'Mtumwa hauwawi' kazi yake ni kufikisha alichotumwa na mtumaji, yaani hanaga mbambamba anafikisha kama alivyotumwa nami acha niwafikishie salamu zenu kwenye sikukuu yenu hapo Lupaso.

Ni shughuli nzito chini ya Mc wa kimataifa Ramadhani Kayoko, huyu atawalinda vema, 'si mmemlipa?' na miiko ya kazi yake ni kuwapamba na mazuri yenu na kuwaonya kwa jeuri zenu basi tupeni raha ya macho na hisia za moyo.

Wananchi mwambieni DJ wenu Profesa Nabi awapigie kibao cha :Akiba haiozi', nyie si wababe, nyie si hamnaga mbambamba na 'derby' basi chezeni kibao chenu, katikeni mayenu, mchezesheni mtani chorus yenu hapo sebuleni kwenu.

Wanathiiimba waswahili wanasema
'Asifuye mvuwa imennyea' si imenyesha? si imewalowanisha na suit zenu za Ligi ya Mabingwa, basi isifuni kama hamna mahema ya kujingika na uteja wenu kwa mtani wenu.

Vipi jeans la Guadiola mnene limekauka maana mmemchezesha kibao cha kwao, waja leo waondoka leo lakini kaja juzi, jana kawapa furaha huko chumbani kwenu namba (11 CAF CL), watani wanalia na vibao anavuowapigia, wanaona wivu na tabasamu lenu.

Watani eeeh, Mimi mtumwa tu, sitaki kuongeza chumvi, ila niwakumbushe kuwa 'Asiyekubali kushindwa si mshindani' hayo ni waswahili wamenituma basi chezeni kwa heshima.

Pasuaneni kwa maneno, katikeni kwa nyondo kwa ulumbi wa Chama na Funguo,  zikipigwa beti za Mayele tetemeni na pigeni salute kwa Jenerali akiwasimamisha vitini, ila msijisahaulishe 'Dua la kuku halimpati mwewe'

Nisiwasahau mlio ndani ya vina na vilai, mlio nyuzi na base, mlio vitunguu na hoho, karoti na mdarasini, iriki na viazi,
'Kazi mbaya siyo mchezo mwema' acheni ubaya tupeni biriyani wenye kushiba washibe, waroho wavimbiwe.

'Kufa kwa mdomo mate hutawanyika' ni suala la muda tu semezaneni, tanianeni sana, ila msisahau kuna mmoja mate yatatawanyika ndio kifo cha mdomo.

'Mwana Simba ni Simba' hata kama atalishwa majani, hata kama atakonda bali atabaki kuwa Simba, basi wenye Simba msimtafute mchawi mikichezeshwa kitunisia.

Na nyie Wananch, Mjenga Nchi ni Mwananchi, msije mkakimbia nchi yenu kisa ugumu wa maisha, kuweni wapole kunyweni chai ya pilipili kutoka Tanga na MIgebuka ya Kigoma.

'Mwenye Nguvu mpishe' kwaherini watan, naondoka mie mtumwa tu msiniue yakiwakera.

No comments:

Post a Comment

Pages