HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 31, 2023

Tido: Hali mbaya ya uchumi katika vyombo vya habari chanzo kushuka kwa maadili

IKIWA zimepita siku chache tangu  Waziri Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye kuunda kamati kwa ajili ya kutathimini hali ya uchumi kwa vyombo vya habari, mwenyekiti wa kamati hiyo Tido Mhando amesema hali mbaya ya uchumi katika vyombo hivyo inachangia waandishi kufanya kazi nje ya maadili na misingi halisi.



Akizungumza jijini Dar es Salaam leo katika Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo, Tido amesema hali ya uchumi katika vyombo vya habari imezidi kuwa mbaya na kusababisha kampuni nyingi za habari kufa na zingine kuingia kwenye matatizo.


"Hali inazidi kwenda mrama na kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa mbaya sana kiuchumi, kampuni nyingi za habari zimekuwa katika matatizo makubwa, tumefika mahali waandishi wapo kwenye chombo flani lakini miezi mitatu, minne hadi sita hawajalipwa ila yupo anafanyakazi,  hili linafanya waandishi kwenda hata nje ya maadili na misingi halisi ya uaandishi wa habari,”amesema Tido.

Amesema katika kipindi cha miezi mitatu walichopewa watahakikisha wanaifanya kazi hiyo kwa umakini ili kutatua changamoto hiyo na watatoa mapendekezo mzuri  ambayo wanaimani serikali itayafanyia kazi kwa haraka.

Hata hivyo Tido amewataka waandishi wa habari kote nchini kuwa na imani na kamati hiyo kwamba itakwenda kufanya yale yaliyoyatamani kwa muda mrefu ili kuwa na Tanzania yenye vyombo vya habari imara.


"Nakumbuka wakati waziri alipotangaza kamati hii, baadhi ya waandishi wa habari waliuliza kwa kusema ya kwamba hawa walioteuliwa wote ni viongozi hivyo hawazani kama wataweza kujua hali halisi ambayo wanahabari wanapitia.


"Mimi nipende kuwaondoa wasiwasi huo na kuwahakikishia waandishi wa habari wenzetu kwanza sote sisi tumetokea huko lakini sisi tunaumia sana na haya yanayoendelea kwani ni sawasawa na baba wa nyumba inafika siku ya sikukuu hawezi kununua chakula au kulipa ada ya shule hili linakera sana," amesema Tido

Tido alisisitiza kuwa wapo tayari kuifanya kazi hiyo kwa sababu ni muhimu kwao hivyo wataivalia njuga kwa sababu wao ni wanatasnia na mambo hayo ambayo wizara imewaelekeza kuyafanya yamekuwa yakiwasumbua kwa muda mrefu.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mohamed Abdulah amesema kamati hiyo itakuwa na jukumu la kupata taarifa juu ya hali ya vyombo vya habari  nchini kiuchumi na kiutendaji.

"Hapo tunategemea tupate taarifa ya kina inayoonesha hali ya kiuchumi ya vyombo vya habari, lakini jukumu lingine ni kupata taarifa juu ya hali ya waandishi wa habari katika vyombo hivyo wakiwemo walioajiliwa, vipato vyao, wenye mikataba ya kazi, wawakilishi mikoani na wengine wanaochangia," amesema 

Abdulah amesema jukumu lingine la kamati hiyo ni kutoa mapendekezo ya nini sasa kifanyiÄ·e kwa lengo la kuboresha maslahi ya waandishi wa habari nchini.


"Pia watakuwa na jukumu la kutathmini sababu za changamoto za kiuchumi katika vyombo vya habari, hapo tunategemea kamati hii itabainisha chanzo kikubwa na vinginevyo vya changamoto ya kiuchumi katika vyombo vya habari, watapendekeza njia bora za kukabiliana na changamoto hizi," amesema

Kwa upande wake msemaji wa Serikali Gregson Msigwa amesema vyombo vya habari kipindi cha nyuma vilipiti hali ngumu lakini kupitia kamati hiyo watu wamekuwa na matumaini ikiwemo wawekezaji katika sekta hiyo.


Januari 24, mwaka huu Waziri Nape aliunda kamati hiyo kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kutoridhishwa na uchumi wa vyombo vya habari na waandishi wa habari ambapo aliagiza wizara kuona namna ya kushughulikia jambo hilo na kulifanyia utatuzi.


Kufuatia maelekezo hayo Wizara hiyo iliunda kamati ya watu nane ikiongozwa na Tido ambaye ni mwenyekiti, Gregson Msigwa Katibu, na wajumbe ambao ni Dk. Rosse Rubeni, Joyce Mhavile na Sebastian Maganga


Wajumbe wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communictions L.T.D Bakari Machumu, Kenneth Sembeya Jackiline Owiso na mwandishi wa habari Richard Mwaikenda.

No comments:

Post a Comment

Pages