HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 03, 2023

KITUO CHA AFRIKA MASHARIKI CHA MAFUNZO YA ULINZI NA USALAMA WA VIMELEA CHAFUNGULIWA NCHINI

 

Na. Catherine Sungura,Dar es salaam


Serikali itaendelea kuboresha huduma za Maabara zote nchini kwa kuzingatia matakwa ya ulinzi na usalama wa Kibiolojia na kuhakikisha usalama wa watenda kazi pamoja na mazingira yote kwa ujumla.


Hayo yamesemwa   leo Aprili 3, 2023   na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa hafla ya ufunguzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii kuwa kituo cha Kikanda  cha Afrika Mashariki cha Mafunzo ya ulinzi na usalama wa vimelea jijini Dar es Salaam.


Waziri Ummy amesema kuwa Serikali inafanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha usalama wa afya za Watanzania na wote waishio ndani ya mipaka ya Tanzania inalindwa. “Wizara inatekeleza viwango vya Kitaifa na Kimataifa kuhakikisha vimelea hatarishi vinavyotokana na hatua za upimaji na tafiti ndani ya maabara  havisambai katika jamii na kuleta madhara  kama vile milipuko ya magonjwa”.


Amesema kuteuliwa kwa kituo hicho kunadhihirisha jinsi maabara ya Taifa ya Jamii inaendelea kauminika duniani na kuwa na uwezo wa kupima vimelea vyote hatarishi kwa kuwa vimelea hatarishi vinaweza kutoka kwa wanyama kwenda kwenye mazingira na baadaye  kuathiri afya ya binadamu.


“Utekelezaji wa afua ya ulinzi na usalama (Biosafety and Biosecurity) ni suala mtambuka  baina ya Wizara mbalimbali nchini hivyo tunahitaji kuwajengea uwezo wataalamu wetu, kupitia kituo hiki tutapata fursa ya wataalamu  wetu  wa Tanzania kupata mafunzo ya kimataifa kwa gharama nafuu kwani mafunzo hayo yatakuwa yanafanyika hapa hapa nchini”. Aliongeza Waziri Ummy.


Aidha, Waziri Ummy amesema tangu kutangazwa kwa kituo hicho wamekwishapokea maombi toka Chuo Kikuu cha Musinde Murilo nchini Kenya ya kuleta wanafunzi wanaochukua shahada  ya ulinzi na usalama wa vimelea kwa ajili ya elimu kwa vitendo na kudhihirisha kwamba maabara inaaminika na inayo uwezo.


Hata hivyo Waziri huyo amewashukuru wadau wa Afrika CDC pamoja na wadau wa maendeleo kwa ushirikiano  wenye tija na thamani kubwa kwa Watanzania na kuwataka waendelee kutimiza wajibu wao ili sekta ya afya iendelee kuimarika kwa huduma bora kwa wananchi.


Naye, mwakilishi kutoka Afrika CDC Dkt. Talkmore Maruta ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwazi wa kutoa taarifa hususani ya ugonjwa wa Marburg na hivyo kuonesha namna nchi inakuwa salama na  na kuongeza kuwa CDC itaendelea kushirikiana  na Serikali na kuwajengea uwezo  wataalamu wa afya nchini  katika kujiandaa, kutambua na kukabiliana na magonjwa ya milipuko.


Tanzania  inaungana na nchi ya Afrika ya Kusini  ambayo imekwishateuliwa kuwa kituo cha mafunzo kwa nchi za kusini mwa Afrika ambapo Tanzania iliwasilisha maombi ya kuteuliwa  kuwa kituo cha maombi mnamo Septemba  2022 na Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ilipata asilimia 100.

No comments:

Post a Comment

Pages