HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 28, 2023

TANTRADE YASHUHUDIA UTIAJI SAINI WA MKATABA WA MAKUBALIANO KATI YA TBA NA PUM NETHERLAND

MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeshiriki kikamilifu  na kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa makubaliano ya kibiashara  kati ya  Chama cha Uokaji Tanzania (TBA) na kampuni kutoka uholanzi (PUM Netherland) uliofanyika katika Ubalozi wa  Uholanzi  jijini Dar es Salaam.  



Mkataba huo ni matunda yaliyopatikana Kutokana na uhusiano mzuri wa kibiashara na uwekezaji uliopo kati ya Tanzania na nchi ya Uholanzi  utakaosaidia kuleta mapinduzi katika sekta ya Uokaji Tanzania, ambapo timu ya  wataalamu kutoka Uholanzi inatarajiwa kuja Tanzania  kutoa  mafunzo mbalimbali kwa wadau wote wa uokaji na kuwasaidia kutengeneza bidhaa zenye ubora na  viwango vinavyokubalika kimataifa.

Akizungumza mara baada ya makubaliano hayo, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Wiebe De Boer amesema kuwa Serikali ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika  kuboresha mazingira ya uwekezaji katika  sekta ya Viwanda na sekta nyingine, hivyo  kwa hali hiyo imewasaidia wao kama balozi kuweza kuleta wawekezaji wengi  kuja kuwekeza Tanzania.

 ‘’Tunahaidi kuwa tutasaidia sekta ya uokaji Tanzania kuwa na   mabadiliko makubwa na kuchochea uchumi na pato la Taifa, pia huu ni mwanzo unaofungua milango ya mikataba mingine mingi zaidi ya kibiashara,  hivyo nawapongeza sana TBA kwa kupata fursa hii ya kufanya kazi na Ubalozi wa Uholanzi, Umoja huu utasaidia kuboresha mahusiano mazuri ya kibiashara yaliyopo kati ya Tanzania na Uholanzi" amesema De Boer.

Naye Mwenyekiti wa TBA, Fransisca amesema kuwa, makubaliano hayo yamehusisha  wataalamu kutoka Uholanzi kuja  kutoa  mafunzo mbalimbali kwa wadau wote wa uokaji Tanzania na kuwasaidia kutengeneza bidhaa zenye ubora na  viwango vya hali ya juu.

Amesema wataalamu hao wanatarajiwa kuwasili Tanzania  katika jiji la Dar es salaam  June, 2023 na baadae katika jiji la Arusha Agosti, 2023,  ili kutoa elimu na mafunzo ya uokaji wa vitafunwa mbalimbali.

‘’Kwa sasa tunaanza kutoa elimu ya uokaji kwa watu wote,  baadae tutaingia  mpaka mashuleni kuwapatia Wanafunzi elimu hii itakayowasaidia kuwajenga kiakili na kimaarifa, na pia elimu hii itasaidia kuleta ajira kwa vijana wengi, ivyo natoa wito kwa Watanzania kuangalia fursa zilizopo katika Tasnia hii  ya uokaji," amesema

Kwa upande wake Ofisa Biashara kutoka TanTrade, Fredy Liundi akimuakilisha Mkurugenzi Mkuu Latifa Khamis, amesema kuwa, ikiwa ni moja kati ya shughuli  za TanTrade ambazo ni  kusaidia wajasiliamali na wafanyabiashara katika kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi.

Amesema TanTrade imefanya kazi kwa ukaribu na TBA na kuwaunganisha na wajasiliamali mbalimbali na kuwapatia  mafunzo ya uokaji  ambayo yamewasaidia katika shughuli za ukuzaji uchumi binafsi na nchi kwa ujumla,  hivyo mkataba huo utasaidia kuinua sekta ya uokaji na kuchochoa uchumi wa Tanzania.

‘’Serikali ya Tanzania,  inatambua mchango mkubwa wa sekta ya uokaji katika kuzalisha ajira na kuchochea uchumi, hivyo hatuna budi kuwaunga mkono na kuwapa nguvu waokaji wa Tanzania  ili kuhakikisha kuwa sekta ya uokaji inaendelea kukua na kupata mafanikio’’ amesema Liundi.


No comments:

Post a Comment

Pages