HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 27, 2023

TMA: Ni miezi mitatu ya baridi, upepo



Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a akielezea hali ya msimu wa kipupwe utakaoanza Juni hadi Agosti mwaka huu.


Na Mwandishi Wetu


KAIMU Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang'a amesema maeneo mengi ya nchi yatapata joto la chini kati ya nyuzi joto 13oC na 19oC kwa kipindi cha Juni, Julai na Agosti.


Dk. Chang'a ameeleza hayo leo Mei 26,2023 kwenye taarifa yake kuhusu msimu wa kipupwe unaoanza Juni, Julai na Agosti (JJA) na kwamba hali hiyo itaambatana na upepo kiasi kwenye maeneo mengi ya nchi hivyo kuwatakwa wananchi kuchukua hatua.


Taarifa hiyo imeeleza kuwa,  hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa kuwepo katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini -Magharibi na ukanda wa Ziwa Victoria huku vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza Juni.


"Maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu) wanatarajiwa kuwa na baridi la wastani hadi joto kiasi.


"Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 13 oC na 19 oC," ilisomeka sehemu ya taarifa ya Dk. Chang'a.


Hata hivyo ukanda wa Pwani ya Kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba) imeelezwa kuwa hali ya joto kiasi hadi baridi la wastani linatarajiwa kwenye maeneo mengi.


Kwa mujibu wa taarifa ya kaimu mkurugenzi huyo, kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 22oC na 26oC kwa maeneo ya mwambao wa Pwani na visiwani wakati nyuzi joto 19oC na 22oC linatarajiwa maeneo ya nchi kavu.


Taarifa hiyo inasema maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 19oC.


"...Kanda ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara) hali ya joto kiasi hadi baridi la wastani linatarajiwa katika maeneo mengi na kiwango hicho kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 13oC hadi 21oC.


"Hata hivyo, maeneno yenye miinuko kwa mikoa hiyo yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 13oC.


"Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma) Dk. Chang’a ameeleza hali ya joto kiasi hadi baridi la wastani linatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini litakuwa kati ya nyuzi joto 15oC na 19oC.


"Kwa Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma) hali ya joto kiasi hadi baridi la wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 14oC na 19oC.


"Ukanda wa pwani ya kusini  (Mikoa ya Mtwara na Lindi) amesema hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 16oC na 22oC," ilisomeka hivyo sehemu ya taarifa kutoka kwa Dk. Chang'a.


Imeelezwa kuwa kanda ya kusini (Mkoa wa Ruvuma) inatarajiwa kuwa na hali ya joto kiasi hadi baridi la wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 11oC na 16oC.


Ukanda ya Nyanda za juu Kusini-Magharibi (Mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na maeneo ya kusini ya Mkoa wa Morogoro TMA imeeleza hali ya baridi la wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 7oC na 16oC.


Hata hivyo, taarifa hiyo imebainisha kuwa maeneo ya miinuko kwenye mikoa hiyo, kiwango hicho kinatarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto 7oC.


Kuhusu mwenendo wa upepo kwa kipindi cha JJA, taarifa ya Dk. Chang’a imeeleza kuwa kawaida msimu wa Kipupwe hutawaliwa na upepo wa Kusi.


"Msimu wa JJA, 2023 unatarajiwa kuwa na upepo utakaovuma kutoka kusini-mashariki na mashariki (Matlai) katika ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.


“Kwa ujumla, upepo wa wastani unatarajiwa kushamiri katika maeneo mengi nchini,” imeeleza taarifa hiyo.


Kuhusu mwelekeo wa mvua kwa kipindi cha JJA Dk. Chang’a amesema kwa kawaida kipindi cha JJA kinatawaliwa na hali ya ukavu katika maeneo mengi ya nchi.


Imeelezwa kuwa upepo kutoka Kusini-Mashariki hadi Mashariki unatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika Bahari ya Hindi ambao unaweza kusababisha vipindi vya mvua katika maeneo machache ya ukanda wa pwani (mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment

Pages