WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michezo ya Dunia kwa watu wenye ulemavu wa akili wameondoka kuelekea Ujerumani kushiriki michezo hiyo itakayoanza Juni 17 hadi 26.
Msafara huo wa
watu 27 umeondoka saa moja asubuhi ya leo, wakipanda ndege ya Shirika la
Turkish, ukiwa na matumaini makubwa ya kurejea na medali na zawadi
nyingine nyingi katika mashindano hayo.
Kwa mujibu
wa kocha Mkuu wa timu hiyo, Deogratius Mdemu kikosi chake kilichoweka
kambi ya wiki mbili jijini Arusha kina ari ya kufanya vizuri na kubeba
medali za dhahabu katika michezo ya riadha na mpira wa Wavu.
Mdemu alisema watanzania wawaombee dua njema ili wafanye vizuri katika michezo hiyo ya Dunia.
Naye
Matron wa wachezaji hao Saada Hamad Ali ameiomba serikali kuwapokea kwa
shangwe zaidi pindi watakaporejea kutoka Ujerumani na ushindi wa aina
yake.
Alisema mara nyingi kwenye michezo ya
Kimataifa, Tanzania hufanya vizuri ambako mwaka 2019, kwenye michezo ya
Dunia iliyofanyika Abu Dhabi Falme za Kiarabu, Tanzania walikuwa
Mabingwa wa mpira wa Wavu.
Aidha hivi karibuni
Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dk Pindi Chana wakati anaikabidhi
bendera ya Taifa timu hiyo alisema Serikali imedhamiria Tanzania kufanya
vizuri kwenye michezo ya Kimataifa.
Chana alisema
hiyo inaendana na miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan tumeshuhudia
timu za Simba na Yanga zikifanya vizuri kwenye michezo ya Klabu bingwa
Afrika na Shirikisho.
Kama hiyo haitisho timu ya
Walemavu wa viungo ya Tembo Worries iliyoshiriki mashindano ya Dunia
nchini Uturuki na timu ya Taifa ya wasichana 'Serengeti girls'
iliyoshiriki Kombe la Dunia nchini India.
Waziri
Chana alisema katika michezo hiyo ya Dunia nchini Ujerumani itashuhudiwa
na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi sambamba na Mawaziri wenye
dhamana ya michezo bara na Zanzibar.
Msafara huo
ulioelekea Ujerumani unaongozwa na makocha watatu akiwemo, Mdemu,
Stephen Oloo na Agustino Shamte huku viongozi wengine ni Mkuu wa msafara
ni Dk Mwanandi Mwankemwa, Mwakilishi wa wazazi Shamsa Diwani.
Wachezaji
watakaoipambania nchi ni Sheha Hamad, Abdulrahmani Shabani (Kigamboni),
Neverson Minja (Arusha), Herith Suleimani (Kiongozi wa wachezaji),
Nassor Juma (Zanzibar) na Mathias Makanyaga (Geita).
Wengine ni Luqman Sabri (Temeke), Duncan Lucian na Ibrahim Mabeche (Kigamboni) na Oswald Kipoto (Kinondoni).
Kwa
upande wa wasichana ni Fatuma Omari (Kigamboni), Shakira Omari na
Johari Mohamed (Temeke), Rebeka Chales, Elizabeth Simon na Aziza Mussa
(Arusha), Dorcas Julius na Sarah Kagoma (Kinondoni), Recho William
(Tanga) na Maimuna Juma (Zanzibar).
No comments:
Post a Comment