HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 15, 2023

MAONESHO YA 18 YA ELIMU YA JUU, MAMBO YAMEIVA


Na John Marwa


MAONESHO ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, yanatarajiwa kuanza Julai 17 hadi Julai 22 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.


Akitangaza tarehe ya kuanza kwa maonesho hayo, leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa amesema maonesho ya mwaka huu yanapambwa na kauli mbiu ya 'Kukuza ujuzi nchini kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwa uchumi imara na shidani'.



"Rasmi tunatangaza maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia haya yanatarajiwa kuanza tarehe 17 Julai, siku ya jumatatu na yatakamilika Julai 22, 2023 katika viwanja vya Mnazi Mmoja.


"Maonesho ya mwaka huu yanapambwa na kauli mbiu ya 'Kukuza ujuzi nchini kupitia Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia kwa uchumi imara na shidani. 


"Niwaombe Wananchi wote wa ngazi mbalimbali, wafanyabiashara, wenye viwanda, waajiri binafsi, nitoe wito waweze kuhudhuria katika maonesho haya, watakutana na Taasisi zetu za Elimu ya Juu na tunatarajia takribani Taasisi zaidi ya 80 zitakuwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo wataonyesha kazi zao mbalimbali ambazo wanafanya, wataonyesha huduma zao za ushauri wanazozitoa na huduma nyingine mbalambali."Amesema Prof. Kihampa na kutoa wito.



"Lakini nitoe wito pia kwa waombaji wa Shahada ya kwanza katika mwaka wa masomo 2023/2024 na wazazi, walezi kuweza pale watakapopata nafasi kuhudhuria maonesho haya kwa sababu Taasisi za Elimu ya Juu zinazofanya udahili nazo zitakuwepo pale.


"Taasisi hizi pia zitakuwa zinatoa ushauri, lakini baadhi yao watakao kuwa tayari wataweza kufanya udahili hapo hapo katika viwanja vya Mnazi Mmoja kwa sababu zaidi ya huduma ambazo Taasisi hizi zitatoa itakuwepo pia ya kufanya udahili kwa shahada ya kwanza kwa mwaka 2023/2024." Amesema, Prof. Kihampa


Hata hivyo sherehe za uzinduzi wa Maonesho hayo zitafanyika Julai 18 viwanjani hapo ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.

No comments:

Post a Comment

Pages