Na John Marwa
MSHAMBULIAJI wa Wekundu wa Msibazi Simba, Mosses Phiri ametangaza hali ya hatari kwa mabeki wa timu pinzani za Ligi Kuu Soka Tanzania Bara NBC PL msimu huu kwani amejipanga kufunga mabao zaidi kama akiendelea kupata nafasi ndani ya kikosi cha timu hiyo kwa msimu wa 2023/24 wa mashindano.
Katika mchezo wa juzi Phiri aliingia dakika ya 53 na kufunga bao lake la kwanza katika mechi yake ya pili ya Ligi akiingia uwanjani kuchukua nafasi ya Jean Baleke, dhidi ya Dodoma Jiji FC, uliopigwa uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Phiri amesema amefurahi sana kufunga bao lake la kwanza kwenye mechi hiyo kwani ni jambo lililomfurahisha kila mwanasimba.
Amesema anafikiria kuendelea kufunga zaidi kila anapopata nafasi ya kucheza na kufanya kile alichokifanya msimu uliopita kwa kufunga idadi ya mabao 10 kabla ya kupata majeraha.
“Nafurahi kucheza mechi yangu ya kwanza na kufunga bao , ninaimani kwa kushirikiana na wenzangu nitawapa furaha mashabiki wa Simba na kuhakikisha tunapambana kufikia malengo wanayoyatarajia ikiwemo kushinda kila mechi.
"Matarajio yangu ni kufunga zaidi kila ninapopata nafasi ya kucheza, msimu uliopita nilifunga mabao 10 na sikuweza kuendelea kwa sababu ya majeraha ninaimani na kumuomba Mungu kunijalia afya njema ili niweze kukata kiu ya mashabiki wetu,” alisema Phiri.
Ameongeza kuwa hawezi kuahidi atafunga mabao mangapi kwa sababu matarajio yake na wenzake ni kuhakikisha msimu huu mashabiki wao wanapata furaha kwa kupambana kusaka poiti tatu muhimu kwa kila mechi."
"Bado niko hapa, nina mkataba na hii timu na ntaendelea kuwa mwaminifu kwenye hii klabu, kuhusu nafasi ya kucheza mwalimu ndiye anaamua nami ntaendelea kutii programu ya mwalimu na atakapo kuwa ananipa nafasi basi ntaitumia kuwafurahisha mashabiki wetu." amesema Phiri.





No comments:
Post a Comment