HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 09, 2023

Njaa yakumba milioni 300

Na Selemani Msuya

 

WATU milioni 333 barani Afrika wanakabiliwa na njaa na utapiamlo, hivyo imeelezwa kilimo kinachozingatia Sayansi na Teknolojia ndivyo pekee vinaweza kuwaokoa na kadhia hiyo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia ya Kilimo Afrika (AATF), Dk Canisius Kanangire kwenye utoaji tuzo za Waandishi Bora wa Sayansi na Teknolojia Afrika (OMAS 2023).

 

Nchini tuzo hizo zimeandaliwa na Jukwaa la Bioteknolojia ya Kilimo Afrika (OFAB), AATF na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

 

Tuzo za mwaka huu, zilitolewa Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, huku mshindi kwa Tanzania akiibuka mwandishi Lucy Ngowi wa Gazeti la Habari Leo, na mshindi wa Afrika akiwa Tinsae Habte Sibane wa Ethiopia.

 

Dk Kanangire alisema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya Waafrika milioni 333 wamekumbwa na njaa na utapiamlo, hivyo njia ya kuwakwamua na janga hilo ni kujikita kwenye kilimo kinachozingatia Sayansi na Teknolojia.

 

Mkurugenzi huyo alisema kuna kasi ya mabadiliko ya tabianchi duniani, hivyo AATF kwa kushirikiana na wadau imeanzisha tuzo za uandishi wa habari za sayansi na kilimo teknolojia kama njia kuhamasisha kilimo kitakacho kabiliana na njaa na utapiamlo.

 

Alisema utafiti unaonesha njia zingine zinazotumika katika kilimo zimeshindwa kusaidia wakulima, hivyo ni vema nguvu zikaelekezwa kwenye kilimo teknolojia kwani kimeonesha kumudu kukabiliana na changamoto za mkulima.

 

“AATF ilianza mwaka 2014 kutoa tuzo kwa waandishi wa habari za sayansi na kilimo, ambapo mwaka huu ni za tisa, lengo ni kuona kundi hili linahamasisha viongozi  na wakulima kujikita katika kilimo cha kutumia Sayansi na Teknolojia, kwani kwa hali ilivyo sasa ya mabadiliko ya tabianchi, ni ngumu mkulima kufanikiwa kwa mbinu za kizamani,” alisema.

 

Dk Kanangire alisema iwapo wakulima watajikita kwenye Sayansi na Teknolojia kwenye kilimo, ni wazi changamoto ya njaa na utapiamlo itaisha Afrika.

 

Alisema tuzo hizo zilianzishwa na OFAB kwa kushirikiana na AATF zikihusisha nchi 11 za Afrika za Malawi, Rwanda, Msumbiji, Kenya, Uganda, Tanzania, Burkina Faso, Nigeria, Ghana, Ethiopia na Afrika Kusini.

 

Meneja Mradi wa OFAB, Vitumbiko Chinoko alisema tangu kuanzishwa tuzo hizo, zaidi ya waandishi 250 wameshiriki katika ngazi ya nchi wanachama na zaidi 150 wakishiriki ngazi ya Bara la Afrika.

 

Alisema jitihada zao ni kuona idadi ya waandishi wa habari wenye kuandika habari za kupigania sekta ya kilimo ikiongezeka, huku akisisitiza utafiti kufanyika ili kuendeleza sekta ya kilimo.

 

“Sisi tunajisikia faraja, kwani mradi huu umekuwa ukipanuka siku hadi siku na imani yetu ni siku moja kuona nchi za Afrika zinajikita kwenye Sayansi na Teknolojia, ili kumkomboa mkulima,” alisema.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Mkenda alisema Serikali inatambua mchango wa wanahabari, katika kutangaza teknolojia zinazochangia mabadiliko endelevu ya kilimo Afrika.

 

Alisema tuzo za OMAS kwa waandishi na vyombo vya habari ni msingi mzuri wa kufanya kundi hilo kuelimisha umma faida za kilimo cha teknolojia.

 

“Kupitia mawasiliano yenye ufanisi na uandishi unaowajibika, bioteknolojia ina uwezo wa kuleta mapinduzi kwenye kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuboresha maisha ya jamii zetu,” alisema.

 

Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu alisema tuzo hizo zinalenga kuhamasisha uandishi wa habari za kisayansi upande wa kilimo, ili kuisaidia jamii kupata tafsiri kirahisi na kufahamu maudhui yanayokusudiwa ili kuongeza uzalishaji wenye tija.

No comments:

Post a Comment

Pages