Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakuna mwananchi asiye na sifa ambaye ameandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura Zanzibar kama inavyodaiwa na ACT Wazalendo na hawajasikia lalamiko la mwananchi yeyote kuwa hakuandikishwa katika daftari hilo ambalo lilianza 07 hadi 13 Oktoba 2024.
Akizungumza na wanahabari, Unguja 27 Septemba 2025, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Zanzibar, Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema muda uliwekwa kwa mujibu wa sheria na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (ZEC) na wale ambao walikuwa na malalamiko yoyote au pingamizi waliwasilisha katika muda ambao ulipangwa.
Alisema sheria ya uchaguzi ya mwaka 2018 kifungu namba 4 kinasema mtu yeyote atakuwa na sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura iwapo ni mZanzibari aliyefikisha miaka 18 na ataandikishwa iwapo ataonyesha kitambulisho chake cha Ukaazi kinachotolewa chini ya sheria husika.
“Mtu yeyote awe Mmasai, Mnyamwezi aliyetimiza vigezo vilivyoainishwa ana haki ya kupata kitambulisho cha Ukaazi toka kwa Sheha ambayo yupo kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa na cha kupigia kura kwa aliyekidhi vigezo” alisema Mbeto.
Mbeto alisema kifungu cha 4 cha sheria hiyo kinaeleza wazi kuwa mtu ambaye kwa madhumuni ya sifa ya ukaazi, hana sifa ya kuandikishwa katika jimbo alilopo sasa anaweza kurejea jimbo lake la zamani na kuandiklishwa kuwa mpiga kura kama ilivyotokea kwa Mwenyekiti na mgombea Urais Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman ‘OMO’.
Mwenezi Mbeto alifafanua kuwa OMO alishindwa kujiandikisha kwa mara ya kwanza kama mpiga kura mpya Mbweni na Kikwajuni Bosnia anakoishi na akakubalika eneo la Mpendae alipokuwa akiishia zamani alikokidhi vigezo na hiyo imefanyika kwa mujibu wa sheria za uchaguzi zilizopo.
Mbeto alisema madai kuwa kuna watu wa jamii ya Maasai wameandikishwa kupiga kura ni hoja isiyo na mashiko kwa kuwa kuna ambao wapo toka miaka ya tisini wakati serikali ilipoamua kuita uwekezaji katika sekta ya utalii hivyo walikuja kwa makundi kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo za ulinzi wa mahoteli.
“Kuna ambao wana zaidi ya miaka 30 Zanzibar vipi leo isemwe kuwa eti hawana sifa, tume ina vigezo vyake na imevitumia kuwaandikisha wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura akiwemo yeye OMO” alisema Mbeto.



No comments:
Post a Comment