HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 28, 2025

Othman Masoud: Uchumi wa Zanzibar Utapanuka Tukitumia Rasilimali za Bahari kwa Ufanisi

Mgombea Urais wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kuligeuza zao la bahari, hususan biashara ya dagaa, kuwa sekta rasmi na yenye mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Zanzibar.

Akizungumza na wavuvi na waanikaji wa dagaa katika eneo la Mangapwani, Wilaya ya Kaskazini B, Unguja, Othman alisema rasilimali za bahari za Zanzibar zimesalia kuwa wimbo wa kisiasa bila utekelezaji, jambo linalowanyima wananchi fursa ya kufaidika moja kwa moja.

“Dagaa ni biashara kubwa sana inayoweza kuingiza kipato kikubwa kwa wananchi wetu na kusaidia kukuza uchumi wa nchi. Lakini kutokana na mifumo mibovu, wageni ndio wanachukua nafasi huku wavuvi wetu wakiendelea kunyanyaswa,” alisema Othman.

Mgombea huyo aliongeza kuwa Serikali ya ACT Wazalendo itahakikisha wavuvi na waanikaji wa dagaa wanawekewa mazingira bora ya kufanya kazi zao, ikiwemo mabanda ya kisasa ya uanikaji, miundombinu ya kuhifadhi mazao ya baharini, pamoja na ufuatiliaji wa bei halisi ya bidhaa hiyo katika soko la dunia.

“Ni jambo la kusikitisha kuona wafanyabiashara wetu wanaendelea kuanika dagaa chini kwa kutumia mabusati na jua pekee. Hii ni dhahiri kuwa wakati wa mvua hakuna biashara inayofanyika.

" Serikali yangu itageuza sekta hii kuwa rasmi na kuhakikisha dagaa la Zanzibar linauzwa kote duniani,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Othman alisema Serikali ya ACT Wazalendo itawawezesha wananchi kupitia mikopo nafuu isiyo na vikwazo, ili kuwaendeleza wafanyabiashara wadogo na wa kati, hususan wale wanaotegemea bahari kama nyenzo kuu ya kipato chao.

Wakazi wa Mangapwani walionesha matumaini makubwa kufuatia ujio wa mgombea huyo. Ali Makame Issa, mmoja wa waanikaji wa dagaa, alisema: “Kwa miaka yote niliyofanya shughuli hii, sijawahi kumuona kiongozi wa Serikali au mgombea kufika hapa. Ujio wa Othman Masoud unaonesha ni kiongozi wa watu na anapaswa kupewa nafasi.”

Naye Maimuna Abdalla, mwanamama anayejishughulisha na uanikaji dagaa, alisema: “Mazingira tunayofanyia kazi ni magumu mno, wakati mwingine tunakata tamaa na kujiona kama sio sehemu ya Wazanzibar. Lakini leo tumepata matumaini mapya kupitia Othman Masoud.”

Kwa kauli hizi, Othman Masoud ameendelea kuimarisha taswira yake kama mgombea anayejali wanyonge na anayeona katika sekta za kiasili kama vile bahari nyenzo muhimu za kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa Zanzibar.






No comments:

Post a Comment

Pages