HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 09, 2025

Mbeto:Tutamlinda Rais Samia kwa gharama yoyote

Na Mwandishi  Wetu, Pemba

Chama Cha Mapinduzi kimeahidi kitawalinda kwa gharama yoyote  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein  Ali Mwinyi  dhidi ya vibaraka na mamluki wachache wanaotishia amani na umoja wa Kitaifa nchini. 


Pia  CCM kimesema hila na njama za wakorofi    wowote hazitafua dafu kwani watanzania muda wote   wako madhubuti. 

Katibu  wa Kamati  Maalum  ya NEC  Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi  Mbeto Khamis ameitaja  thamani ya uhuru na umoja wa Kitaifa ulioasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere  na mwenzake  Sheikh Abeid  Amani Karume vitalindwa kwa nguvu zote. 

Mbeto alisema  serikali za CCM hazitingishwi na makundi ya wanasiasa au weanaharakati wasiojitambua kwa tamaa ya kupata  fedha. 

Alisema kila atakaejaribu kuchezea amani, utulivu na mshikamano uliopo  nchini , atakiona chamtema kuni na kilichomtoa kanga manyoya.

"Watanzania Hawajalala, bado wako macho na makini  muda wote, Hawatawatupa mkono Rais  Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi dhidi ya vitisho  vya wanasiasa waliokubali kuupiga mnada utu wao" alisema Mbeto.

Katibu  huyo Mwenezi alisema wanasiasa  na Wanaharakati wenye nia ya  kuiweka rehani amani ya Taifa letu, watakabiliwa na mwisho wa  aibu na fedheha isiokadirika  .

"Wasifikiri kwa  wao kwa kununuliwa kwao na vipande vya sarafu nao  wangeweza kuwanunua watanzania. Toka sasa kila mmoja wao ajitafakari na kusalimu amri . Watanzania  waganga njaa" alieleza.

Katibu huyo Mwenezi alisema CCM kwa wakati huu kikiendelea na  kampeni  zake nchini kinawataka waTanzania kutobabaishwa na propaganda za bei rahisi katika mitandao ya kijamii badala yake wachapekazi  na kuzalisha mali.

"Ifikapo Oktoba 29 mwaka huu  wananchi  tokeni ,  nendeni mkapige kura vituoni bila  longolongo. Nendeni mkatimize matakwa ya  kikatiba, kiraia na kidemokrasia "alisisitiza.

Pia Mbeto aliwataka watanzania  kila mmoja atumie haki yake ya kuchagua  bila kupoteza  kura na kuwachagua wagombea  wa CCM, Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.  

"Uchaguzi  utafanyika. Matokeo yatatangazwa , washindi watajulikana , maisha baada ya uchaguzi  yataendelea kama kawaida " alisema Mbeto.



No comments:

Post a Comment

Pages