Dar es Salaam. Serikali imesema kuwa asilimia 50 ya bajeti ya maendeleo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeelekezwa katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya kati na elimu ya juu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha vijana kupata ujuzi na maarifa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Daniell Mushi, wakati akitoa hotuba yake katika Kongamano la Kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere lililojadili Falsafa yake katika kujenga Amani na Mshikamano wa Kitaifa.
Prof. Mushi amesema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya serikali ya kuhakikisha vijana wanapata elimu yenye tija itakayowawezesha kujiajiri na kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira ya elimu na mafunzo ya ujuzi, huku akisisitiza kuwa mafanikio ya mtu mmoja mmoja yanahitaji juhudi binafsi sambamba na fursa zinazotolewa.
Aidha, amebainisha kuwa kumekuwepo na maboresho ya mitaala yanayolenga zaidi elimu ya ujuzi (amali) ili kuzalisha wahitimu wenye stadi mbalimbali zinazohitajika katika soko la ajira.
Pia, amesema bajeti ya mikopo ya wanafunzi na ufadhili wa masomo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, hatua inayolenga kupanua upatikanaji wa elimu kwa vijana wengi zaidi.
Akihitimisha, Prof. Mushi ametoa wito kwa Watanzania kushirikiana na serikali, taasisi pamoja na sekta binafsi kuendeleza misingi ya amani na mshikamano iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, huku akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua kwa vitendo katika kujenga taifa lenye maendeleo endelevu.




No comments:
Post a Comment