DAR ES SALAAM
Benki ya CRDB pamoja na kampuni zake tanzu imekutana na wateja wake pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo wanahisa, wawekezaji, sekta binafsi na sekta ya umma katika Jukwaa la Wawekezaji lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema lengo la jukwaa hilo ni kuimarisha ushirikiano na wadau ili kukuza uchumi na kuongeza uimara wa taasisi hiyo.
Amesema benki hiyo inaendelea kujikita katika kutoa huduma bora kwa Watanzania pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi.
“Tumekutana na wadau wetu kujadili namna bora ya kushirikiana katika kukuza uchumi na kuifanya taasisi yetu kuwa imara zaidi huku ikiendelea kuwafikia watu wengi zaidi. Tunaamini maendeleo endelevu ya taasisi yanapatikana kupitia ushirikiano wa karibu na wadau wetu,” amesema Dk. Nsekela.
Aidha, amesema benki hiyo imeendelea kuwahamasisha vijana kuwekeza katika hisa pamoja na kuwawezesha kutimiza ndoto zao za kijasiriamali kupitia huduma mbalimbali za kifedha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Neema Mori, amesema jukwaa hilo limelenga kuwaeleza wadau safari ya maendeleo ya benki hiyo pamoja na mipango yake ya baadaye.
Prof. Mori amesema CRDB imekuwa ikitekeleza mpango mkakati wake kwa mafanikio katika kipindi cha miaka minne iliyopita, huku ikiendelea kuboresha huduma kwa wateja na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali.
“Tumewashirikisha wadau wetu kuhusu mafanikio yetu ya mwaka 2025/26, maono yetu ya baadaye, pamoja na namna tunavyoendelea kuzingatia sera zinazohusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi kupitia huduma endelevu za kifedha,” amesema Prof. Mori.
Ameongeza kuwa benki hiyo inaendelea na mikakati ya kupanua huduma zake ndani na nje ya Tanzania ili kuwafikia wananchi wengi zaidi pamoja na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi.




No comments:
Post a Comment