HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

May 16, 2026

CRDB Yaendelea Kung’ara Sekta ya Fedha Nchini

Na Mwandishi Wetu

Benki ya CRDB imeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika sekta ya fedha nchini kwa kuimarisha ukuaji wa uchumi, kuongeza mikopo kwa sekta binafsi na kupanua huduma zake kimataifa.

Akizungumza wakati akifungua Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB katika Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa hao, uliobeba kauli mbiu ya “Vijana na Uwekezaji kwenye Hisa” inayofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar alisema kuwa haiwezekani kuzungumzia mafanikio ya sekta ya fedha nchini bila kuitaja CRDB kutokana na mchango wake mkubwa katika kuunganisha akiba za wananchi, mitaji ya wawekezaji pamoja na mahitaji ya maendeleo ya uchumi.



Alisema takribani asilimia 29 ya mikopo kwa sekta binafsi nchini hutolewa na CRDB, jambo linalodhihirisha nafasi kubwa ya benki hiyo katika kukuza shughuli za kiuchumi nchini.

Aidha, alisema matokeo ya uendeshaji wa benki hiyo yanaendelea kuimarika ambapo mwaka 2025 CRDB ilipata faida safi baada ya kodi ya shilingi bilioni 725.

“Sina wasiwasi, karibuni mtaweka rekodi mpya ya kufikia shilingi trilioni moja,” alisema.

Kiongozi huyo aliwapongeza wanahisa wa CRDB kwa kuendelea kuiamini Bodi na Menejimenti ya benki hiyo, hatua iliyowezesha kutolewa kwa gawio kubwa zaidi kuwahi kutolewa na CRDB.

Pia aliipongeza benki hiyo kwa kuendelea kubuni bidhaa mbalimbali za kifedha ikiwemo ushiriki katika Samia Infrastructure Bond kwa kushirikiana na TARURA, hati fungani za kijani pamoja na bidhaa zinazozingatia misingi ya Sharia kama Sukuk.



Alisema ubunifu huo unaonesha uwezo wa sekta ya fedha nchini kuhamasisha mitaji kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu, uchumi wa kijani na ujumuishi wa kifedha.

Katika hatua nyingine, CRDB imeendelea kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa kupitia uwepo wake nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku maandalizi yakiendelea kuingia katika masoko ya Kenya na Zambia.

Uzinduzi wa Ofisi ya Uwakilishi ya CRDB nchini Dubai, Falme za Kiarabu, umeelezwa kuwa hatua muhimu katika kuiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika ushindani wa kimataifa wa huduma za fedha.

Hatua hiyo inatarajiwa kuwasaidia wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania kufanya shughuli zao kwa urahisi zaidi ndani na nje ya nchi.




No comments:

Post a Comment

Pages