HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

June 29, 2026

CRDB Insurance Company yaleta bima ya kidijitali kwa wafuga ng’ombe

Kampuni ya CRDB Insurance Company ikishirikiana na Agriculture and Climate Risk Enterprise (ACRE Africa) imezindua Smart Mifugo, bima inayotumia akili mnemba kuwalinda wafugaji dhidi ya hasara hususan zile zitokanazo na vifo vya ng’ombe.

Akizindua huduma hiyo inayopatikana kupitia Programu ya DigiBima,   jukwaa la kidijitali linaloratibu usajili, uuzaji na usimamizi wa bima za kilimo na mifugo kwa wakulima na wafugaji barani Afrika kwa kutumia simu au kishkwambi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye idadi kubwa ya mifugo, jambo linaloifanya sekta hii kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.

Amesema sekta ya mifugo inatoa ajira na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa chakula, kipato cha kaya, na maendeleo ya viwanda vinavyotegemea mazao ya mifugo ingawa kuna changamoto zinazoikabili yakiwemo magonjwa, majanga ya asili kama ukame na mafuriko na hatari nyinginezo zinazosababisha hasara kwa wafugaji wetu.

“Nafurahi kuona ushirikiano wa CRDB Insurance Company na ACRE Africa umeleta teknolojia ya kisasa kulinda mali za wafugaji wetu. Kupitia Smart Mifugo, wafugaji sasa wanaweza kupata bima kwa njia ya kidijitali kwa urahisi zaidi, tena salama na ya uwazi. Matumizi ya akili mnemba katika kutambua alama ya pua ya mnyama, ni hatua kubwa sana katika maendeleo ya sekta hii. Ubunifu huu utasaidia kuongeza uaminifu, kupunguza udanganyifu, na kuboresha utoaji wa huduma za bima,” amesema Agnes.



Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuleta ubunifu utakaoongeza tija katika uzalishaji na kuboresha maisha ya wananchi akisisitiza kuwa Smart Mifugo inaendana na jitihada za Serikali za kuimarisha maendeleo ya sekta ya mifugo, kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, na kuifanya sekta hii kuwa ya kisasa na yenye ushindani zaidi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela amesema wameleta ubunifu huo kwa kutambua kwamba sekta ya mifugo ni mhimili muhimu wa uchumi wa taifa na chanzo cha kipato kwa mamilioni ya Watanzania hivyo kustahili mazingira salama.

“Wafugaji wetu wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa mfumo madhubuti wa kutambua umiliki wa mifugo. Hali hii inawanyima fursa ya kupata huduma muhimu kama bima na mikopo. Kuanzishwa kwa Smart Mifugo ni hatua ya kimkakati ya kukabiliana na changamoto hizo kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Kupitia huduma hiyo, ng’ombe hutambuliwa kwa kutumia alama ya pua (cow muzzle biometrics), ambayo hutofautiana kati ya mnyama mmoja na mwingine,” amesema Dkt. Nsekela.

Ubunifu huo, amesema unaondoa utata wa umiliki wa mifugo, unaongeza uaminifu katika utoaji wa huduma za bima na kuwezesha mifugo kutambulika rasmi kama mali yenye thamani inayoweza kutumika kama dhamana kupata mikopo. Dkt. Nsekela amesema baada y auzinduzi huo, huduma hii itapatikana katika mataifa yote ambako Benki ya CRDB inatoa huduma yaani Burundi na Congo pia ambako kuna idadi kubwa ya mifugo.

Wakati Smart Mifugo ikiwapa wafugaji uhakika wa usalama wa mifugo yao dhidi ya hasara na kuwawezesha kuwatumia ng’ombe wao kama dhamana ya kupata mikopo benki, Dkt. Nsekela amesema huduma hiyo itachochea ukuaji wa sekta ya mifugo, kuongeza uwekezaji, kupanua ujumuishaji wa kifedha hususan vijijini, na kuimarisha usalama wa chakula.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance Company, Wilson Mnzava amesema ushirikiano wao na ACRE Afrika unaung amkono dhamira ya Benki ya CRDB kuendeleza ubunifu wa kifedha unaolenga kujenga uchumi jumuishi na endelevu nchini.

“Tunachoanza leo ni mwanzo tu. Tunaanza na ng’ombe, lakini tuna matarajio makubwa ya kupanua huduma hii kwa aina nyingine za mifugo kadri tunavyoendelea,” amesema.

Kwa wafugaji wanaohitaji huduma hii, Mnzava wanaweza kuipata katika tawi lolote la Benki ya CRDB hivyo akawaomba wadau kuchangamkia fursa hii ya kuilinda mifugo dhidi ya majanga tofauti kwa uchumi imara wa familia na jamii nzima ya wafugaji kwa ujumla.



Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ACRE Africa, Ewan Wheeler amesema Tanzania ina takriban ng’ombe milioni 40 wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 4.5 ila sehemu kubwa ya utajiri huu upo kwenye sekta isiyo rasmi hivyo kuhitaji mikakati ya pamoja na kuirasmisha.

“Wafugaji wanahangaika sana kupata bima na mikopo kwa dhamana ya mifugo yao kutokana na ugumu wa kuitambua lakini kwa kutumia akili mnemba jambo hilo limepata suluhisho sasa hivi. Kwa kurahisisha utambuzi wa mifugo, taasisi za fedha zitakuwa na Imani kubwa ya kurudisha fedha zao hivyo kuwakopesha wafugaji watakaokuza ufugaji na kuongeza tija ya sekta ya mifugo nchini,” amesema Wheeler.











No comments:

Post a Comment

Pages