HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

June 03, 2026

CRDB Yazindua Mikopo ya Hadi Milioni 300 Kidijitali Bila Dhamana

 Dar es Salaam, Juni 3, 2026 – Benki ya CRDB imezindua maboresho makubwa katika huduma zake za mikopo, yakimuwezesha mteja kupata mkopo wa hadi Shilingi milioni 300 kidijitali bila hitaji la dhamana wala mdhamini.



Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili, alisema kuwa huduma hiyo mpya inalenga kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wateja kwa kutumia teknolojia ya kidijitali.

Alieleza kuwa mteja anaweza kuomba mkopo huo kupitia simu ya mkononi, kompyuta mpakato (laptop) au kwa kuingia kwenye mfumo wa Employee Self Service (ESS), ambapo atachagua Benki ya CRDB na kufuata hatua chache za maombi.



“Mkopo huu hauhitaji dhamana wala mdhamini. Mteja hahitaji kukutana na afisa mikopo wala kutembelea tawi la benki. Anaingia kwenye mfumo, anaomba na ndani ya muda mfupi anaweza kupata mkopo wa hadi Shilingi milioni 300,” alisema Adili.

Aliongeza kuwa huduma hiyo ni sehemu ya mageuzi makubwa ya kidijitali katika sekta ya huduma za kifedha, tofauti na miaka ya nyuma ambapo kupata mkopo wa kiwango hicho kulihitaji mchakato mrefu wa kujaza nyaraka, kutafuta wadhamini na dhamana mbalimbali.

“Zamani kupata mkopo wa Shilingi milioni 300 ilikuwa safari ndefu yenye urasimu mkubwa. Leo hii mteja anaweza kupata mkopo huo kwa urahisi kupitia simu yake au kompyuta kwa kubofya hatua chache tu,” alisisitiza.

Aidha, Adili amesema kuwa kuanzia Juni 4, waombaji wa mikopo hiyo watakuwa wanapata majibu ya maombi yao papo hapo bila kulazimika kupiga simu au kufanya ufuatiliaji wowote.



“Haya ndiyo mapinduzi ya huduma tunayoyaleta kupitia Benki ya CRDB. Tunataka wateja wetu wapate huduma kwa haraka, kwa urahisi na kwa usalama zaidi,” alisema.

Maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa wafanyakazi na wateja wanaostahili, huku yakichochea matumizi ya huduma za kifedha kidijitali nchini.



No comments:

Post a Comment

Pages