NA EDITHA WILLIAM, BUKOBA KAGERA
Wamiliki wa ardhi na viwanja mkoani Kagera wametakiwa kuviendeleza ili kuepusha migogoro ya ardhi na uvamizi unaoweza kujitokeza kutoka kwa watu wasiokuwa waaminifu.
Hayo yameelezwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Kagera, Bw. Erick Makundi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu umuhimu wa kutunza ardhi pamoja na njia sahihi za kuchukua kwa mwananchi anapokumbana na changamoto za ardhi.
Bw. Makundi amesema kuwa wamiliki wa ardhi ambao wameviendeleza viwanja vyao si rahisi kwa watu wengine kuvamia maeneo hayo kwani tayari yanaonesha umiliki halali.
Amebainisha kuwa wananchi wanaomiliki ardhi wanapaswa kulinda mipaka ya maeneo yao kwa kuzingatia masharti yaliyopo kwenye nyaraka za umiliki walizopewa ili kuepuka madhara na migogoro inayoweza kujitokeza baadaye.
Aidha, amesema kuwa ipo mifumo maalumu ya kutatua migogoro ya ardhi, ikiwemo mifumo ya kiutawala na mifumo ya kisheria kupitia Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji, Kata, Wilaya pamoja na Mahakama za Ardhi. Amewataka wananchi kufuata taratibu hizo rasmi wanapokumbana na migogoro ya ardhi ili kupata haki kwa mujibu wa sheria.
Pia amesisitiza umuhimu wa wananchi kuwa na utamaduni wa kufuatilia na kuhifadhi nyaraka zao za umiliki wa ardhi ili kurahisisha utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza.





No comments:
Post a Comment