HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

June 07, 2026

JASMINE NG'UMBI AIOMBA SERIKALI KUANZISHA BENKI MAALUM YA VIJANA

NA DENIS MLOWE- MAFINGA, IRINGA


MBUNGE wa Viti Maalum anayewakilisha Vijana, Jasmine Ng'umbi, ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha benki maalum kwa ajili ya vijana ili kuwawezesha kupata mikopo yenye riba nafuu na hivyo kuongeza fursa za kiuchumi kwa kundi hilo muhimu katika maendeleo ya taifa.


Jasmine alitoa ombi hilo alipokuwa akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, katika mkutano wa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi uliofanyika katika Uwanja wa Wambi mjini Mafinga, Mkoa wa Iringa.


Katika hotuba yake, Jasmine alimpongeza Waziri Mkuu kwa ziara yake ya kutembelea majimbo yote ya Mkoa wa Iringa na kusikiliza changamoto za wananchi, akisema ziara hiyo imeonesha dhamira ya Serikali ya kuwahudumia wananchi na kuhakikisha maendeleo yanafika katika maeneo yote.

"Ninatambua kazi kubwa uliyoifanya katika mkoa wetu wa Iringa. Vijana wa mkoa huu tunafurahia juhudi zako pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan," alisema.

Alisema miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Iringa imeendelea kufungua fursa kwa vijana na kuwafanya kuwa sehemu ya nguvu kazi ya taifa.

Jasmine alieleza kuwa Serikali imeendelea kuwashika mkono vijana kupitia mipango mbalimbali ya kiuchumi, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa makundi maalum.

Alibainisha kuwa katika Wilaya ya Mufindi, vikundi zaidi ya 30 vya vijana vimenufaika na mikopo hiyo katika miaka ya fedha ya 2024, 2025 na 2026, huku vikundi 21 vya wanawake na vikundi 10 vya watu wenye ulemavu navyo vikifaidika.

Alisema mahitaji ya mikopo hiyo yameendelea kuongezeka kutokana na idadi kubwa ya vijana wanaohitaji mitaji ya kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi.

"Uhitaji wa mikopo hii ni mkubwa mno. Tunaomba Serikali ilione suala la kuanzisha benki maalum ya vijana kwa jicho tofauti ili kuwasaidia kupata mikopo yenye riba nafuu na kwa urahisi zaidi," alisema.

Pia alimpongeza uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa juhudi za kuhakikisha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wanapata mikopo ya asilimia 10 kwa wakati.

Mbali na suala la mikopo, Jasmine aligusia changamoto zinazowakabili vijana wanaojishughulisha na sekta ya usafirishaji katika Wilaya ya Mufindi, akisema wengi wao wamejiajiri au kuajiriwa katika shughuli za usafirishaji na hivyo kukabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji ufumbuzi wa Serikali.

Alisema vijana hao wana mchango mkubwa katika uchumi wa eneo hilo na taifa kwa ujumla, hivyo ni muhimu Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya kazi na biashara kwa sekta hiyo.

Mkutano huo ulikuwa sehemu ya ziara ya Waziri Mkuu katika Mkoa wa Iringa yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Pages