Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Benki ya CRDB imewahimiza Watanzania kuendelea kutumia huduma ya SimBanking huku ikieleza kuwa matumizi ya huduma hiyo yameongezeka kwa kiwango kikubwa tangu kuanza kwa kampeni ya SimBanking Kimpango Wako.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa droo ya robo mwaka ya kampeni hiyo, Meneja wa Huduma za Kibenki kupitia Simu ya Mkononi, Amina Mawona, alisema benki imefurahishwa na mwitikio mkubwa wa wateja ambao umechangia kuongezeka kwa idadi ya miamala inayofanyika kupitia SimBanking.
Alisema katika droo ya robo mwaka, wateja watano waliojishughulisha na miamala kupitia SimBanking wamejishindia safari ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Aidha, katika kundi la wateja waliotumia huduma za mawakala kwa miamala ya kuanzia Shilingi 10,000, washindi 11 walipatikana ambapo mshindi mmoja alijishindia jokofu la milango miwili, huku washindi wengine 10 wakijishindia runinga janja (Smart TV) za inchi 65.
Mawona alisema kampeni hiyo itaendelea hadi mwezi Desemba mwaka huu, ambapo mbali na zawadi za kila wiki na kila robo mwaka, kutakuwa na zawadi kubwa ya mwisho wa mwaka kwa washindi watakaofanya vizuri zaidi.
Alieleza kuwa washindi hao watapatiwa safari ya siku saba barani Ulaya kutembelea nchi mbalimbali, wakiwa pia watapatiwa Shilingi milioni moja kila mmoja kwa ajili ya matumizi binafsi, huku gharama zote za safari na bima zikigharamiwa na benki.
Kwa mujibu wa Mawona, kila wiki kampeni hiyo hutoa zawadi kupitia makundi matatu. Kundi la kwanza linahusisha wateja wanaofanya miamala kupitia SimBanking, ambapo washindi 50 hupata Shilingi 20,000 kila mmoja. Kundi la pili ni wanafunzi 10 wanaotumia SimBanking, ambao pia hujishindia Shilingi 20,000 kila mmoja.
Aliongeza kuwa kundi la tatu linawahusisha wateja wanaofanya miamala kupitia mawakala kwa kuanzia Shilingi 10,000, ambapo washindi 33 huchaguliwa kila wiki. Kwa ujumla, kampeni hiyo huzalisha takribani washindi 93 kila wiki na zaidi ya washindi 470 wa zawadi mbalimbali kwa kipindi cha mwezi.
Mawona aliwataka Watanzania kuendelea kutumia SimBanking katika kufanya miamala yao ya kila siku ili kuongeza nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali zinazotolewa kupitia kampeni ya SimBanking Kimpango Wako.




No comments:
Post a Comment