Na Ripota wa TBN, Arusha
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amewashauri wajumbe wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kuimarisha usimamizi wa bajeti na utekelezaji wa sera za afya ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Zungu ametoa ushauri huo Oktoba 8, 2026, akifungua mdahalo kuhusu afya ya mama na mtoto ulioandaliwa na Serikali ya Tanzania kwa wajumbe wa Mkutano wa 153 wa IPU, unaoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Amesema mabunge yana wajibu wa kutunga sheria, kutenga fedha za kutosha na kusimamia matumizi yake ili rasilimali zifike kwenye huduma za afya na jamii zinazozihitaji.
Zungu amesisitiza kuwa afya na ustawi wa wanawake, watoto na vijana ni msingi wa maendeleo ya taifa. Ameeleza kuwa ni muhimu kuimarisha huduma za mama na mtoto mchanga, afya ya uzazi, lishe na ustawi wa vijana, huku hatua za kisiasa zikilenga kuondoa vikwazo vinavyozuia wananchi kupata huduma hizo.
“Kipaumbele chetu kiwe kwenye upatikanaji sawa wa huduma, ikiwemo huduma za mama na mtoto mchanga, afya ya uzazi, lishe, na afya na ustawi wa vijana,” amesema Zungu.
Kwa upande wake, Mshauri wa Rais anayeshughulikia masuala ya afya, ustawi wa jamii, wanawake na watoto, Ummy Mwalimu, amesema Afrika imepiga hatua katika kupunguza vifo vya kina mama, ingawa maendeleo hayo bado hayatoshi.
Ummy amesema vifo vya kina mama katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika vilipungua kwa asilimia 42 kati ya mwaka 2000 na 2023. Hata hivyo, Afrika bado inachangia takribani asilimia 70 ya vifo hivyo duniani. Ameonya kuwa kwa kasi ya sasa, bara hilo linaweza kufikia lengo la vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000 karibu mwaka 2050.
Washiriki wa mdahalo huo wamejadili pia umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi na chanjo kwa watoto, na kuhakikisha ahadi za kisiasa zinageuzwa kuwa sheria, bajeti na usimamizi unaofikisha huduma kwa wananchi.
October 09, 2026
Home
Unlabelled
ZUNGU AWASHAURI WAJUMBE WA IPU KUIMARISHA USIMAMIZI WA BAJETI ZA AFYA
ZUNGU AWASHAURI WAJUMBE WA IPU KUIMARISHA USIMAMIZI WA BAJETI ZA AFYA
Share This
About HABARI MSETO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Author Details
Ut wisi enim ad minim veniam, quis nostrud exerci tation ullamcorper suscipit lobortis nisl ut aliquip ex ea commodo consequat. Duis autem vel eum iriure dolor in hendrerit in vulputate velit esse molestie consequat.




No comments:
Post a Comment