Naibu Mkurugenzi Uchaguzi na Mipango wa CUF, Shaweji Mketo akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu kuteswa kwa wanachama watano wa chama hicho na askari wa JWTZ mkoani Mtwara.
Baadhi ya
Viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kutoka (kulia) ni, Mwenyekiti wa Vijana Wilaya ya Mtwara Mjini,
Ismaili Njalu. Katibu wa Wilaya ya
Mtwara mjini, Said Kulanga na Mwenyekiti wa Wilaya ya Mtwara mjini, Salum
Mohamed wakiwaonesha waandishi wa habari majelaha waliyoyapata baada ya
kupigwa na Wanajeshi wa Wananchi (JWTZ) katika mkutano uliofanyika Makao Makuu
ya Chama hicho Dar es Salaam
DAR ES SALAAM, Tanzania
CHAMA cha Wananchi (CUF) kinaandaa utaratibu wa kufungua kesi
mahakamani dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na Wanajeshi wa
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa watendaji wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,Naibu Mkurugenzi Mipango, Uchaguzi wa Bunge Shaweji Mketo,kwa niaba ya wanachama wenzake alisema, bado wanawasiliana na wanasheria, taasisi za
haki za binadamu na mamlaka nyingine ili kupata mwongozo waweze kufungua kesi
hiyo.
Mketo na wenzake watano, ni miongoni mwa watu walioonja
joto ya mateso ya siku 28 kutoka kwa askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ), ambao wameweka kambi Mtwara kudhibiti machafuko yanayotokana na madai
ya kuzuia bomba la gesi asilia lisijengwe Dar es Salaam.
Mbali na Mketo wengine ni Mwenyekiti wa Vijana
Mtwara mjini Salum Mohamed, Mwenyekiti wa Mtwara mjini Salum Mohamed,
Mwenyekiti wa Wilaya Mtwara vijijini Ismail Jamal,Katibu wa Wilaya Mtwara mjini
Said Kulaga na dereva wa CUF makao makuu Kashinde Juma.
Akisimulia mkasa huo uliompata yeye na wenzake alisema wakiwa njiani
walikutana na gari mbili za jeshi kubwa na ndogo zikiwa njia panda ya newala na mtwara mjini,na
kuwasimamisha huku walitokea askari
wapatao 50 vichakani na kuanza kuwapiga huku wakiwasachi mifukoni.
“Askari wa JWTZ walikuwa 50 walitusachi na
kuchukua fedha zangu shilingi 85,000 na nilipoanza kuzuia fedha hizo
wasizichukue ndipo walipoanza kunipiga kweli wakanivua viatu vyangu nilivyowahi
kununua nje ya nchi wakavichukua na mimi kuniachia vyao vya jeshi hivi hapa ,”alieleza
Mketo.
Alisema walikuwa wakipigwa na fimbo, kumwagiwa
maji yaliyokuwa yamewekwa barafu na pilipili jambo ambalo liliwafanya waendelee
kupata maumivu makali sana.
Mketo alisema hata hivyo kuteswa kwao ni ishara
kuwa Mtwara bado inanuka damu na hakuna usalama huku wananchi wengi wakihofiwa
kufariki dunia.
Hata hivyo alisema wakati wakiendelea kuwatesa alisikika
mwanajeshi mmoja akisema wao wapo pale kwa ajili ya kutekeleza amri ya Waziri Mkuu
aliyoitoa Bungeni kwamba wananchi watakaokaidi amri ya serikali wanatakiwa
kupigwa.
Kiongozi huyo ambaye aliongea kwa masikitiko
makubwa huku akiwataka wenzake kuonesha majereha kwa wanahabari alisema kuwa
licha ya kuwaambia wanajeshi waliokuwa wakiwatesa kuwa amefanyiwa upasuaji
mkubwa wasimpige eneo hilo hawakujali kwani waliendelea kumchapa na bakora katika
eneo la mshono hadi lilipogeuka rangi na kuwa nyeusi.
Alisema kiongozi mmoja ambaye ni Mwenyekiti wa
Mtwara mjini Salum Mohamed aliambiwa azivute ndevu zake kwa kutumia mikono na
alifanya hivyo hadi haapo zilipoanza kuvuja damu ndipo wakamwambia walichokuwa
wanakihitaji.
Mketo alisema vitendo hivyo ni vya kinyama na
kwamba haviwezi kuvumilika hivyo serikali inatakiwa kuviangalia utendaji kazi
wa vyombo vya dola kwani ni kulinda raia na si kutesa.
Hata hivyo aliilaumu serikali kwa kuvifungia
vyombo vya habari mkoani humo kwa kigezo cha kwamba vinawashawishi wananchi
kuandamana jambo ambalo si kweli.
No comments:
Post a Comment