WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imeifunga kambi ya Mtabila na kuwaondoa wakimbizi wote kutoka
Burundi baada ya kugoma kufanya hivyo kwa hiari.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya maridhiano ya pande tatu
yaliyofanyika Oktoba 8,mwaka huu huko Geneva ambapo Serikali ya Tanzania,
Burundi na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi Duniani(UNHCR) waliamua kuwaondoa
wakimbizi hao ili kuepusha machafuko,ghasia na vurugu ambazo zingeweza kutokea.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam leo, Waziri mwenye dhamana, Emanuel Nchimbi, alisema kuwa maamuzi hayo
yamefikiwa baada kuonekana raia hao hawaonyeshi nia yeyote ya kurudi nchini
kwao kwa hiari hasa baada ya machafuko kuisha.
Nchimbi alisema katika machafuko ya mwaka 1993 nchini
Burundi kufuatia kuuawa kwa Rais Melkior Ndadaya, Tanzania ilipokea wakimbizi
550,000 hadi kufikia mwaka 2002 lakini wengine waliondoka baada ya machafuko
kuisha na kubaki 36,000.
Alisema kuwa baada ya mwaka huu kutangazwa kwa zoezi la
kurudi kwa hiari ni wakimbizi 1305 ndio waliokubali hali iliyosababisha
serikali kuamua kuwavua hadhi ya ukimbizi waliosalia kwa mujibu wa sheria ya
wakimbizi ya mwaka 1998.
Alisema kuwa baada ya zoezi hilo kushindikana waliamua kuwarudisha
kwao kwa kutumia urejeaji wa kusimamiwa na kubaki 2400 katika kambi ya
Nyarugusu ambao wanasababu za msingi kuendelea kubaki nchini wakisubiri
suluhisho lingine la kudumu.
Aidha alisema kuwa mpaka sasa makambi yote tisa ya wakimbizi
wa nchi hiyo yamefungwa na kueleza kuwa endapo kuna wakimbizi waliotoroka na
kujichanganya uraiani watakamatwa na sheria itachukua mkondo wake na
watahukumiwa kwa sheria ya mwaka 1998.
Nchimbi alisema kuwa baada ya kuifunga, kambi hiyo itafanyiwa ukarabati na sehemu ya majengo yake
yatatumiwa na wananchi pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT).
No comments:
Post a Comment