Mkuu wa Wilaya ya Iringa akizundua Jengo la Utoaji wa Huduma ya Macho katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (Picha zote na Denis Mlowe)
Na Denis Mlowe, Iringa
JUMLA ya shilingi Milioni 105 zatumika katika ukarabati wa
Jengo la Huduma ya upasuaji wa Macho na kati ya hizo milioni 35 zitatumika kwa
gharama ya kununulia vifaa vya tiba ya macho katika hospitali ya rufaa ya
Iringa.
Mkuu wa Wilaya kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Iringa Dk.
Leticia Warioba alisema hayo wakati akizungumza na wafanyakazi na wadau
mbalimbali wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa mwishoni mwa wiki iliyopita
wakati wa uzinduzi wa Jengo la Huduma ya Upasuaji wa Macho na pamoja na Kituo
cha Huduma ya Upimaji na kutengeneza miwani katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa
wa Iringa kwa udhamini wa mashirika ya
Sightsaver na Brien Holder Vision kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Walioba alisema kwamba watumishi wa idara ya afya hususani
upande wa macho kuzingatia kwamba wanatumia msaada huo kwa malengo
yaliyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi na kuwataka wasimamizi wa huduma za afya
hospitalini hapo kuhakikisha kuwa vifaa vyote vilivyotolewa na wadau kuingizwa
katika leja ya Hosptali ya Mkoa.
“Vile vile vifaa hivi vitunzwe kwa kufanyiwa matengenezo na
kinga kama inavyotakiwa ili viweze kutoa
huduma kwa muda mrefu” alisema dk. Warioba na kuongeza kwamba “Ushirikiano
ambao mashirika haya yameonyesha katika kuboresha huduma za afya ya macho ni
mfano wa kuigwa na wadau wengine wa sekta za huduma za jamii”
Awali mratibu wa huduma ya macho katika Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Iringa Dk. George Kabona alisema kwamba lengo la mradi huo ni
kuhakikisha watu wote wenye upofu unaozuilika wanapata huduma na wale wenye
upofu usiozuilika hasa watoto wanapata elimu bora kuhusu huduma za macho.
Alisema kwamba jumla ya watu 725 waliokumbwa na mtoto wa
jicho walifanikiwa kufanyiwa operesheni toka mwaka 2009 hadi 2011 na
opereshi zote walifanyiwa watu 1265 kati
ya wagonjwa 22,169 waliojitokeza ndani ya miaka mitatu ya 2009/2010/2011
aliongeza kusema kuwa mradi huo umewezesha kuwajengea uwezo watoa huduma wa
macho mbalimbali ndani ya mkoa ikiwemo madaktari watatu wa upasuaji wa mtoto wa
jicho ambao wawili wanatoa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
“Mradi umeweza kutoa elimu kwa wahudumu wengi wa afya ya
msingi katika zahanati zetu ili waweze kutoa hudma nzuri za macho hasa maeneo
ya vijijini ambako wataalam wa macho hawapatikaniki” alisema Dk. Kabona
Mradi Jumuishi wa Huduma za macho mkoani Iringa ulianzishwa
mwaka 1998 kwa kushirikiana kati ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa chini ya
Katibu Tawala wa Mkoa na Shirika lisilo la kiserikali la Sightsaver.
No comments:
Post a Comment