HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 29, 2013

WAFANYABIASHARA KARIAKOO WALALAMIKIA KUCHELEWESHWA MIZIGO YAO BANDARINI

 Na Mwandishi Wetu, 

BAADHI ya wafanyabiashara katika maduka ya nguo Kariakoo jijini Dar es Salaam wameendelea kulalamika, pamoja na kuelezwa kuwa suala lao la kucheleweshwa mizigo yao Bandarini linashughulikiwa na serikali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini leo, wamesema 'kuwa hadi sasa hawajui kilichongumzwa kwenye kikao kilichowahusisha Waziri wa Fedha, Mkuu wa Mkoa, Kamishna Mkuu wa TRA, Kamanda wa Kanda Maalum na Mwenyekiti wao wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo'.

Mlalamiko yao yote wanayalekeza kwenye Kampuni ya Silent Ocean Limited ambayo ndiyo iliyokuwa wakala aliyekuwa akiwaingizia mizigo yao kutoka katika baadhi ya nchi za Asia.

Mmoja wa wafanyabiashara hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Masao alisema wakala huyo ameshindwa kutekeleza makubaliano yao ya awali ya kupakuwa mzigo huo kwa zaidi ya miezi minne sasa hali inayowaweka katika wakati mgumu ambao unawafanya waingie kwenye mgogoro mwingine na taasisi za fedha kwa kushindwa kulipa mikopo waliyokopa.

“Unajua kuna siri ambayo tumeipata tunasikia kuna baadhi ya Kampuni wakati kabla ya Waziri Mwakyembe kupewa Bandari kulikuwa na mchezo kwa baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wakiingiza makontena ya nguo kama vile vitenge lakini wakijidai yamefungasha mzigo kama sidiria, tai, saruji vitu ambavyo kodi yake iko chini wakati wakijua fika wanaibia serikali”alisema Masao. 

Masao alisema ugumu wa upakuzi wa mizigo yao iliyokuwa ikiingizwa na kampuni hiyo ulianza mara Waziri wa Uchukuzi, Harryson Mwakyembe alipokabidhiwa waizara hiyo.

Alisema waziri huyo ambaye kutokana na dhamana aliyopewa ilimfanya aweze kubadili uongozi wa Bandari ambao ulikuwa ukidaiwa kujihusisha kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyabiashara katika kukwepa kodi.

Mwenyekiti wa Umoja huo, Mathias Makoi, akitolea ufafanuzi malalamiko ya wafanyabiashara hao, kwanza alikiri kukwama kwa makontena hayo Bandarini.

Hata hivyo, alisema katika kumaliza tatizo hilo hivi sasa wako kwenye mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mkurugenzi TRA ambapo mazungumzo hayo yamefikia hatua nzuri.

“Hivi sasa mazungumzo hayo yanaendelea na suala hilo liko kwa mkuu wa mkoa na Kamanda wa Polisi bila ya kufafanua.

“Hapa lilipo tumefikia panatosha na wala hatutaki liandikwe tena kwenye vyombo vya habari, na hatutaki kuyavuruga mazungumzo hayo”alisema Makoi.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Silent Ocean Limited aliyejitambulisha kwa jina la Haleem, alikubali kuchelewa kwa mizigo hiyo lakini kilichosababisha hali hiyo ni mabadiliko ya viwango vya kodi ambavyo hivi sasa vimepanda ukilinganisha na awali.

“Kodi imeongezeka, fikiria kama mwanzo ulikuwa ukilipa sh 2000 ghafla unaambiwa ulipe sh 5000 ni lazima kwanza uanze kujipanga upya hata hvyo tunajadiliana na wafanyabiashara hao kuona ni jinsi gani tunaitoa mizigo hiyo”alisema.

Kuhusu kikao cha Waziri Dk. Mgimwa, Kamishna wa TRA, Mkuu wa Koa Sadik, Kova pamoja na Mawakala, kilikuwa ni kwa ajili ya kujadili jinsi ya kuboresha utendaji ambao wanadhani utachochea kasi ya upakuaji wa mizigo bandarini hapo na si kujadili makontena yake kama ilivyodaiwa na baadhi ya wafanyabiashara.

No comments:

Post a Comment

Pages