Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba (NHC), David
Shambwe akifafanua jambo jijini Dar es Salaam jana, wakati akitoa taarifa za kuundiwa
zengwe kwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Nehemia Mchechu na Bodi ya
Wakurugenzi ya NHC kuhakikisha harejeshwi katika wadhifa huo baada ya kumaliza
muda wake. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa
Mawasiliano na Huduma kwa Jamii, Muungano Saguya na Mkuu wa Kitengo cha
Manunuzi, Hamis Mpinda. (Picha na Francis Dande)
Kaimu Mkuu wa
Mawasiliano na Huduma kwa Jamii, Muungano Saguya akizungumza wakati wa mkutano huo.
Utangulizi: Jumatatu na Jumanne ya
wiki hii, kumekuwa na taarifa zilizochapishwa kwenye moja ya gazeti la
kila siku zikieleza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Nehemia Kyando
Mchechu ameundiwa zengwe na Bodi ya Wakurugenzi ya NHC kwa nia ya
kuhakikisha kuwa harejeshwi tena katika wadhifa huo, hasa baada ya Bw.
Mchechu kumaliza muda wake wa kuliongoza Shirika hili.
Aidha, gazeti
hilo liliwaaminisha umma wa watanzania kuwa mizengwe hiyo inaungwa mkono
na vigogo wa Serikali wakiwemo Wabunge ambao kuwepo kwa Bw. Mchechu
katika Shirika kumewanyima ulaji ikiwemo kupangishwa nyumba za Shirika.
Gazeti lililienda mbali zaidi likidai kuwa Bw. Mchechu amewekewa
masharti magumu na Bodi hiyo ya kumtaka apunguze idadi ya Wakurugenzi wa
Menejimenti ya sasa ya Shirika.
Kwa kuwa habari hizo zimeleta
mtafaruku katika Shirika na zimesababisha umma kuwa na mijadala
mbalimbali juu ya jambo hili, tungependa kuwataarifu umma kuwa taarifa
hizo hazina ukweli wowote, na Shirika la Nyumba la Taifa linapenda kutoa
ufafanuzi kama ifuatavyo:-
1. Kwanza, ifahamike kuwa Bodi ya
Wakurugenzi ya NHC ina miezi miwili tu tangu iteuliwe na Mamlaka husika
na haijawahi kukaa katika kikao chochote kujadili suala la kumuondoa
Mkurugenzi Mkuu na kupunguza Menejimenti ya Shirika iliyopo sasa.
2. Tunapenda kuwafahamisha kuwa
Mkurugenzi Mkuu na Menejimenti ya Shirika bado wana mikataba halali
ambayo haijamalizika muda wake, hivyo hoja ya kuwa Bwana Mchechu na
Menejimenti yake wanaundiwa zengwe baada ya kumaliza muda wao haina
ukweli wowote.
3. Kwamba kutokuwepo kwa Mkurugenzi Mkuu kwenye ufunguzi wa
miradi hakukutokana na kuwepo mizengwe kama ilivyoripotiwa na Gazeti
hili. Bw. Mchechu alikuwa katika likizo yake ya mwaka iliyooanza tarehe
30 Juni na kumalizika Julai 18, 2014. Likizo hii ni stahili halali ya
Bw. Mchechu kama walivyo watumishi wengine wa umma, na hakuichukua
likizo hii kutokana na kuwepo mizengwe ya kumuondoa kama ilivyoripotiwa
na Gazeti hili. Kuanzia tarehe 21 Julai, 2014 Bw. Mchechu yupo kikazi
nje ya nchi na anatarajiwa kuwa ofisini kwake tarehe 28 Julai, 2014.
4. Mwisho, tunapenda
kuwatanabaisha wanahabari kuwa kama ilivyo kawaida yetu, NHC imekuwa na
itaendelea kuwa mstari wa mbele kutoa habari makini kwa vyombo/chombo
chochote cha habari bila kuficha jambo lolote. Hivyo, tunawaomba
muendelee kuitumia vyema fursa hii kupata habari zenye ukweli na zilizo
sahihi kwa jambo lolote mnalohitaji kuufahamisha umma wa watanzania.
Kwa
kufanya hivyo, tutaendelea kuwa washirika wakubwa wa vyombo vya habari,
tukizingatia kuwa vyombo vya habari vina dhima na dhamana kubwa katika
kuleta tija kubwa kwa Shirika na Taifa letu. Aidha, tunawafahamisha
wateja wetu kuwa hakuna mtafaruku wowote uliyopo ndani ya Shirika la
Nyumba la Taifa na kwamba tunaendelea kuwapa huduma zetu zilizo bora
katika sekta ya nyumba tuliyoaminiwa na Taifa kuisimamia.
IMETOLEWA NA:
BW. DAVID SHAMBWE,
KAIMU MKURUGENZI MKUU,
No comments:
Post a Comment