Na Mwandishi Wetu
MSICHANA mwenye umri wa miaka 19 Anna Malongo amekuwa
kivutio kikubwa, katika mkutano wa wajasiliamali wadogowadogo ulioratibiwa na
Taasisi isiyo ya Kiserikali inayojihusisha na masuala ya kilimo (Ansaf), baada
ya kutoa ushuhuda wa maisha yake kupitia utaalamu wa kutengeneza viatu vya
ngozi.
Anna aliyasema hayo katika mkutano huo uliowakutanisha
wajasilimali mbalimbali kupitia kilimo katika Hotel ya Serena Jijini Dar es
Salaam, kuwa yeye anaishi kwa kupitia utengenezaji wa viatu vya ngozi huku
akiwataka wasichana kama yeye kujiamini na kujiajili kuliko kuilalamikia
Serikali kila kukicha.
Alisema, yeye licha ya kukumbana na changamoto mbalimbali
hasa za umeme na maji katika kijiji chao cha Chilolo Mkoani Dodoma, lakini
anapigana kadri awezavyo kuhakikisha anajikwamua na kuyamudu maisha yake, kwani
licha ya kumaliza kidato cha nne hakupata fursa ya kuendelea kusoma hivyo
kupitia mikono yake anatafuta ada ili ajiendeleze.
“Mimi kusema kweli nina historia kubwa mno katika
ujasiliamali huu, nanunua ngozi ya mbuzi sh 3000 ya ngombe sh 8000 na natoa
hata viatu vya sh 70,000 hivyo nawaomba wasichana wenzangu hasa wa vijijini
kama mimi wasikimbilie kuwa wafanyakazi wa ndani wajitume na kufanya kilimo
kinalipa jamani,”alisema Anna.
Mbali na Anna wajasiliamali wengine waliotoa ushuhuda wa
maisha yao kuwa bora kupitia kilimo ni Michael Tarimo anayejihusisha na ukulima
wa mboga mboga ambapo kupitia kampuni yake ya Home Veg-Tanzania anasafirisha
bidhaa zake nchi kama Uholanzi, Ujerumani na nyinginezo.
Akizungumzia mkutano huo wa siku tatu, Mkurugenzi Mtendaji
wa (Ansaf) Audax Rukonge alisema, lengo la kufanya mkutano huo, ni
kuwakutanisha wajasiliamali ambao wameona matunda yake na wale ambao wanatamani
kuingia ila wamejawa na hofu.
“Sisi Ansaf tunaimani kubwa kuwa kilimo ndio uti wa mgogo
wa mtanzania, na hapa leo tumewaleta zaidi ya wajasiliamali 18 ambao
wamenufahika na kilimo, tunaimani kupitia wao vijana wengine watapata fursa ya
kuchangamkia kilimo,”alisema Rukonge na kuongeza kuwa wanatambua wakulima
wanachangamoto mbalimbali ila wao kwa kushirikiana na Serikali wanajitahidi
kuzitatua.




No comments:
Post a Comment