Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete amemteua Mkuu Mpya mmoja wa Mkoa na kuwahamisha vituo vya kazi wengine
sita kuanzia jana, Jumamosi, Desemba 6, 2014.
Taarifa iliyotolewa leo, Jumapili, Desemba 7, 2014 na
Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue mjini Dar es Salaam inasema
kuwa Rais amemteua Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Mkoa wa Arusha, Ndugu Daudi Felix
Ntibenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Ndugu Ntibenda ataapishwa kesho, Jumatatu, Desemba 8,
2014, saa nne asubuhi, Ikulu, Dar Es Salaam.
Taarifa hiyo inasema kuwa wakuu waliohamishwa vituo vya
kazi ni Mheshimiwa Elaston Mbwilo anayehamishwa kutoka Mkoa wa Manyara kwenda
Mkoa wa Simiyu ambako anachukua nafasi ya Mheshimiwa Paschal Mabiti aliyepewa
likizo ya ugonjwa, Mheshimiwa Joel Nkanga Bendera aliyehamishwa Mkoa wa Manyara
kutoka Mkoa wa Morogoro na Mheshimiwa Dkt. Rajabu M Rutengwe anayehamishwa Mkoa
wa Morogoro kutoka Mkoa wa Tanga.
Wengine ni Mheshimiwa Magalula Saidi Magalula
anayehamishiwa Mkoa wa Tanga kutoka Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Mwantumu Bakari
Mahiza anayehamishiwa Mkoa wa Lindi kutoka Mkoa wa Pwani na Mheshimiwa Mhandisi
Evarist B. Ndiliko anayehamishiwa Mkoa wa Pwani kutoka Mkoa wa Arusha.
Wakuu wengine wa mikoa wanaendelea kubakia katika vituo
vyao vya sasa vya kazi.




No comments:
Post a Comment