Timu za Azam, Mtibwa Sugar, Simba na Yanga zitashiriki michuano ya
Kombe la Mapinduzi inayofanyika kisiwani Zanzibar kuanzia Januari 1 hadi 13
mwakani.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa ruhusa kwa
timu hizo kucheza mashindano hayo baada ya kuhakikishiwa na Chama cha Mpira wa
Miguu Zanzibar (ZFA) kuwa kesi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wake
imeondolewa mahakamani.
Kutokana na timu hizo kushiriki Kombe la Mapinduzi, mechi zao za
raundi ya tisa na kumi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitachezwa katikati ya wiki
baada ya kumaliza mechi zao za michuano hiyo.
Hivyo mechi za VPL ambazo hazitachezwa wikiendi hii ni kati ya
Azam na Mtibwa Sugar, Mbeya City na Yanga, na ile kati ya Mgambo Shooting na Simba.
Mechi za wikiendi ijayo zinazopisha michuano hiyo ni kati ya Kagera Sugar na
Azam, Coastal Union na Yanga, Mbeya City na Simba, na Mtibwa Sugar na Tanzania
Prisons.
18
WAPATA BEJI ZA UAMUZI FIFA
Waamuzi 18 wa Tanzania wamepata beji za uamuzi za Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa mwaka 2015.
Idadi hiyo ambayo ni rekodi kwa Tanzania inahusisha waamuzi saba
wa kike. Waamuzi wa kati wa kike waliopata beji hizo ni pamoja na Jonesia Rukyaa
Kabakama aliyechezesha mechi ya Nani Mtani Jembe kati ya Simba na Yanga. Wengine
ni Florentina Zablon Chief na Sophia Ismail Mtongori.
Waamuzi wasaidizi wa kike waliopata beji hizo ni Dalila Jafari
Mtwana, Grace Wamala, Hellen Joseph Mduma na Kudura Omary Maurice.
Kwa waamuzi wa kati wa kiume ni Israel Mujuni Nkongo, Martin
Eliphas Sanya, Mfaume Ali Nassoro na Waziri Sheha Waziri. Waamuzi wasaidizi ni Alli
Kinduli, Ferdinand Chacha, Frank John Komba, John Longino Kanyenye, Josephat
Deu Bulali, Samuel Hudsin Mpenzu na Soud Iddi Lila.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment