Rais Jakaya Jakaya Kikwete akipokea sehemu ya msaada wa
vitabu milioni 2.5 vya hisabati na sayansi kutoka kwa balozi wa Marekani, Mark Childress
wakati hafla iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Mtakuja iliyopo Kunduchi jijini Dar es Salaam. (Picha na Francis Dande)
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mtakuja wakiimba
ngojera wakati wa hafla ya makabidhiano ya vitabu milioni 2.5 vya Hisabati na
Sayansi vilivyotolewa na Serikali ya Marekani kwa ajili ya shule ya sekondari
za Tanzania.
Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amesema shule za
Sekondari 3,551 za Serikali nchini
zimegawiwa vitabu vya masomo ya Sayansi milioni 2.5 kutoka nchi ya
Marekani ili kupunguza uhaba wa vitabu mashuleni.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana katika shule ya Sekondari Mtakuja
iliyopo Kunduchi Dar es Salaam, waliowakilisha shule zote za sekondari nchini
na kusababisha kuongeza idadi ya vitabu kwa uwiano wa wanafunzi wawili kitabu
kimoja na katika shule nyingine mwanafunzi mmoja kwa kitabu kimoja.
Kikwete alisema huo ni muendelezo wa
Sera ya elimu iliyozinduliwa hivi karibuni
katika shule ya msingi Majani ya chai iliyopo Ilala jijini Dar es
Salaam, na kuahidi kuwa tatizo la vitabu mashuleni kwa sasa ni historia.
Alisema changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni ukosefu wa walimu wa sayansi
kwa idadi ndogo ambapo kwa mwaka 2005 kulikuwa na walimu 500 lakini hadi
kufikia mwaka 2014 kuna idadi ya walimu 18,000 wa masomo ya sayansi na wengine
18,000 wakisubiri ajira zao.
Alisema upungufu wa walimu wa sayansi kwa sasa unatokana na vyuo vingi
kukosa nafasi ya kuchukua walimu wengi wa masomo hayo kwa mkupuo lakini jitihada za Serikali zinafanyika
katika kuhakikisha kuwa walimu wanapata nafasi mbalimbali za masomo hasa katika
mataifa ya nje.
Rais Kikwete pia aliendelea na kuwapa walimu ahadi kem kem ikiwa ni pamoja
na kuwajengea nyumba zao mijini na vijijini ,kuongeza ajira katika masomo ya
Sayansi huku akiwataka walimu kujiendeleza katika masomo hayo kwa kuwa huko
mbele ajira zitakuwa za kumwaga.
Akizungumzia shule ya Sekondari ya Mtakuja ambayo ndio ilikabidhiwa vitabu
hivyo kwa niaba ya shule nyingine nchini alisema kuna uhaba wa walimu nane wa
sayansi ambapo alimuagiza Naibu wa
Waziri wa Tamisemi anayeshughulikia elimu Kassim Majaliwa kuhakikisha
shule hiyo inapatiwa walimu wa sayansi.
Hata hivyo aliwataka walimu kutovunjika moyo huku akiwaambia kwamba endapo
atamaliza muda wake wa urais hata Mkewe mama Salma Kikwete ambaye aliambatana
naye atarudi shuleni kufundisha hatua iliyopelekea walimu kushangilia kwa
shangwe.
Naye Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Mark Childress alisema kuna umuhimu
mkubwa wa kuimarisha stadi za msingi kwa wanafunzi ambao ni pamoja na kusoma
,kuandika na kuhesabu ili kuwawezesha kuelewa vyema maudhui ya vitabu hivyo na
kuweza kuvitumia kikamilifu.
Alisema Serikali ya Tanzania na Marekani zinachukua jitihada za pamoja
katika kuweka msingi imara wa stadi mbalimbali kwa kutoa elimu bora,sio tu
katika masomo ya sayansi bali katika kuandika ,kusoma na kuhesabu.
Balozi huyo alisema lengo la Serikali ya Marekani ni kusaidia Tanzania
program mbalimbali zinazolenga kuongeza fursa za elimu kwa wasichana
kumethibitisha kuleta mafanikio makubwa na endelevu ya kiuchumi.
Naye Meya wa Manispaa ya Kinondoni Yusuf Mwenda alisema kuwa awali manispaa
hiyo ilikuwa na shule tano tu lakini hadi sasa kuna shule 49 ambazo ni sawa
sawa na ongezeko la shule 44 sawa na asilimia 840.
Kukabidhiwa kwa vitabu hivyo kunafuatia mradi mwingine kama huo
uliofadhiliwa na USAID hapo mwaka
2008,ambapo kwa kupitia ushirikiano kati ya chuo Kikuu cha South Calorina na
Wizara ya Elimu ya Zanzibar ambapo zaidi
ya vitabu milioni moja na zana nyingine za kujifunzia ziliandaliwa na
kusambazwa visiwani humo.
No comments:
Post a Comment