Mke wa Rais na Mjumbe wa NEC Taifa, Mama Salma Kikwete, akiwafariji familia ya marehemu Bibi Ashura Abeid Faraji, aliyekuwa muasisi wa vyama vya Afro Shiraz na CCM. Mama Salma alikwenda nyumbani kwa marehemu Tibirizi, Chake Chake juzi. (Picha na John Lukuwi)
 
Na Anna Nkinda–aliyekuwa Pemba
 
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amehani  msiba wa muasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bibi  Ashura Abeid Faraji aliyefariki  mwishoni mwa mwaka jana katika kijiji cha Tibirizi wilaya ya Chakechake mkoa wa Kusini Pemba.

Akiwa nyumbani kwa marehemu Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliwapa pole wafiwa  na viongozi wa Chama na Serikali   na kusema kwamba alitambua mchango wa Bibi Ashura  katika kukijenga chama na kuisaidia jamii inayomzunguka.

Alisema ingawa marehemu Bibi Ashura alikuwa na   umri wa  utu uzima lakini hakuchoka kufanya kazi za kukitetea chama chake na kuisaidia jamii inayomzunguka, kwa yale aliyoyafanya anastahili kuigwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chakechake Hanuna Ibrahim Masoud alisema marehemu alikuwa mshauri wa chama na jamii kwa hiyo wamempoteza mtu wa muhimu sana.

“Licha ya kufanya kazi za chama marehemu pia alikuwa anafanya kazi za kijamii ikiwa ni pamoja na kuwa msuluhishi wa matatizo mbalimbali na kutoa ushauri hivyo basi kutokana na utendaji wake alikuwa anakubalika na vyama vyote vya siasa kikiwemo Chama Cha Wananchi (CUF)”, alisema Hanuna.

Mwaka 1954 Bibi Ashura alianza kufanya kazi na chama cha Afro Shirazi Party (ASP) na baadaye CCM hadi mauti yanamkuta alikuwa mjumbe wa baraza la wazee wa CCM na mjumbe wa halmashauri kuu ya mkoa wa Kusini Pemba.

Baadhi ya nyadhifa alizozishika wakati wa uhai wake katika chama na Serikali ni  Naibu Katibu  Mkuu wa kinamama wa ASP mwaka 1974, mjumbe wa baraza kuu la umoja wa wanawake wa Tanzania mwaka 1966-2012 na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa kupitia mkoa wa Kusini Pemba.

Mbunge wa mwanzo wa kuteuliwa wa Zanzibar aliteuliwa na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1981 – 1995 na mjumbe wa baraza la wawakilishi viti maalum vya wanawake kutoka mkoa wa Kusini Pemba mwaka 2005-2010.

Bibi Ashura alizaliwa mwaka 1938 na hadi mauti yanamkuta Novemba 27,2014 nyumbani kwake Tibirizi aliacha  watoto watatu wawili wa kike na mmoja wa kiume, wajukuu 25  na vitukuu 27.

Mama Kikwete alikuwa kisiwani Pemba kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za Maulid ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) zilizofanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari Utaani Kaskazini Pemba.