Na Bryceson Mathias, Morogoro Vijijini
MCHUNGAJI wa Kanisa la Tanzania
Assemblies of God (TAG) Morogoro, James Samson Mabula (Power Mabula), amesema
baada ya kuitwa na Mungu kwenye uchungaji, ndani mwake Mungu amempa wito wa
kukitumikia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza katika mikutano ya kujinadi
baada ya kutia nia ya kutaka kugombea ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kwa tiketi
ya (Chadema), Mabula ambaye aliwahi kuteuliwa na Askofu Mkuu wa TAG, Barnabas
Mtokambali, kuwa Mchungaji Msaidizi wa Kanisa la Bethel Revival alisema:
“Nilipata wito wa kukitumikia Chadema
katika siasa na kujiunga nacho mapema kabisa, kwa sababu ndicho chama pekee
nilichoona kina nia ya dhati ya kuwakomboa Watanzania, na sasa ukiwemo Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA).
“Nikiwa Chadema, baada ya kuona baadhi
ya wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ambao hawamo katika Umoja wa
UKAWA si waadilifu na hawana mzigo wa kuwatumikia wananchi, nimepata wito wa
kutia nia ya kugombea ubunge Morogoro, Chadema inifikirie,” alisema Mabula.
Mabula alisema iwapo Chadema itampa
ridhaa kusimama katika kinyang’anyiro hicho na akashinda ubunge, moja ya mambo
Matano makuu atakayofanya akishirikiana na chama chake ni kuhakikisha
anarudisha kwa wananchi viwanda 11 vilivyouawa na serikali ya CCM.
Aidha, amesema hatua hiyo itakwenda sambamba
na kuhakikisha huduma ya maji inavifikia vijiji vyote 29 vya Manispaa ya
Morogoro, huku akihakikisha anaungana na wabunge wenzake watakaoshinda
kuilazimisha serikali kulinda rasilimali za wananchi zinazoporwa kila kukicha.
Wanachama 11 wa Chadema wametangaza nia
ya kutaka kuwania Jimbo la Morogoro Mjini, ambalo kwa sasa linaongozwa na
Abdul-Aziz Mohamed Abood (CCM), ambapo miongoni mwao yumo mwanasheria
Bathromeo Tarimo, tayari wanapiga jalamba katika kata 29 kujinadi kwa
wanachama ili wakubaliwe na chama.
No comments:
Post a Comment