Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya
mchezo wa Jumamosi kati ya Tanzania dhidi ya Algeria utakaochezwa katika
uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam bei ya chini kuwa ni shilingi elfu
tano (5,000) tu.
Tiketi za mchezo huo zitaanzwa kuuzwa siku ya ijumaa katika vituo
mbalimbali vinavyotumiwa na TFF kuuzia tiketi, ambapo kiingilio kingine
kitakua ni elfu kumi (10,000) kwa viti vya VIP B & C, huku kiingilio
cha elfu tano kikiwa ni kwa viti vya rangi ya Bluu, Kijani na rangi ya
Machungwa.
Wakati huo huo kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’
kinachodhamininiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, kinatarajiwa
kurejea nyumbani kesho Jumatano mchana kwa shirika la ndege la Fastjet
tayari kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo dhidi ya Algeria siku ya
Jumamosi.
Stars iliyoweka kambi nchini Afrika Kusini imekua ikifanya mazoezi
kila siku katika uwanja wa Edenvale, ambapo mpaka sasa wachezaji wote
wapo katika hali nzuri hakuna majeruhi na kila mmoja yupo tayari kwa
mchezo wa Jumamosi.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema vijana wake wapo
vizuri kifaya, kifikra na morali ni ya hali juu “wachezaji wamekua
wakifanya mazoezi kwa nguvu na kuonyesha umakini mkubwa” alisema Mkwasa.
Aidha Mkwasa amewaomba watanzania na wadau wote wa mpira wa miguu
nchini kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti ya kuwashangilia vijana katika
mchezo dhidi ya Algeria Jumamosi, kwani kutawafanya wachezaji kujisikia
wapo nyumbani na kucheza kwa nguvu zaidi.
Wachezaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu
walioshinda kombe la Ligi ya Mabingwa mwishoni mwa wiki na klabu yao ya
TP Mazembe wanatarajiwa kuungana na wenzao kambini kesho jijini Dar ess
alaam.
No comments:
Post a Comment