HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 26, 2016

TFF YATOA TAHADHARI KWA YOUNG AFRICANS SC

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea taarifa juu ya mpango na kauli za baadhi ya viongozi wa Young Africans SC kushawishi mashabiki wao kufanya vurugu dhidi ya warushaji matangazo ya televisheni ya moja kwa moja wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho la Afrika ngazi ya Makundi kati ya Young Africans ya Tanzania na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) utakaofanyika Juni 28, 2016 saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Dar es Salaam.

TFF ikiwa msimamizi mkuu wa mpira wa miguu Tanzania, inawajibika na mara moja inachukua nafasi hii kuwatahadharisha baadhi ya viongozi wa Young Africans, wanachama na mashabiki wao kutofanya hivyo kwani itakuwa ni kinyume na  kanuni za mashindano na mikataba ya udhamini katika hatua hii.

Ikumbukwe kwamba CAF inamiliki asilimia mia moja ya haki za habari na masoko katika ngazi hii ya makundi na jaribio lolote la kukwamisha matangazo ya biashara au utengenezaji na urushaji wa matangazo ya televisheni au ukwamishaji wa shughuli zingine kama hizo kwa CAF au wakala aliyeteuliwa na CAF kutaigharimu klabu mwenyeji si kwa kutozwa faini tu lakini pia uwezekano wa kuondolewa mashindanoni.


Pia TFF inatoa tahadhari hiyo ikiwamo ile ya utamaduni wa kukaa uwanjani ili kuepusha aina yoyote ya vurugu kwenye michezo yake hususani hii ya hatua ya makundi. TFF inafahamu kuwa tayari viongozi wa Young Africans walikwisha kusoma nyaraka na taarifa mbalimbali kuhusu kanuni na masuala ya udhamini kwa timu zinazofuzu hatua ya Nane Bora.Wapenzi wa Yanga wanaombwa kufika kwa wingi na kuishangilia kwa nguvu  timu yao ikiwa ni njia ya kuitia hamasa.Hata hivyo shamrashamra hizo zifanyike kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu za Mpira wa Miguu na sheria za nchi.

Vitendo vya kuashiria vurugu na kufanya vurugu vikithibitishwa katika taarifa ya Mwamuzi, Janny Sikazwe wa Zambia; Kamishna wa mchezo, Celestin Ntangungira wa Rwanda na Mratibu Mkuu Maalumu kutoka Msumbiji, Sidio Jose Mugadza, hatua zake zitachukuliwa dhidi yake ikiwamo KUONDOLEWA KWENYE MASHINDANO. Vilevile vitendo vya kutishia amani,kudhuru mwili au kuharibu mali vitachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za kijinai.

Katika mchezo huo wa kimataifa Na. 107, Mwamuzi Sikazwe atasaidiwa na Jarson Emiliano dos Santos kutoka Angola atayekuwa kwenye mstari wa kulia (line 1) na Berhe O’Michael wa Eritrea atayekuwa upande wa kushoto (line 2) huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni mwamuzi wa akiba.

Wakati huohuo, kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini kinatarajia kukaa siku ya Jumamosi tarehe 2 Julai 2016. Taarifa zaidi itatolewa karibuni.

…………………………………………………………………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA SOKA TANZANIA

No comments:

Post a Comment

Pages