*Ahimiza elimu kwa mtoto wa kike, akemea mimba za utotoni
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa
mkoa wa Tabora wawapeleke watoto wao shule na waache kuwatumia kama vibarua
kwenye mashamba ya tumbaku.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumapili, Agosti
13, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na
viongozi wa wilaya ya mkoa huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo
maalum.
“Ninasisitiza kuanzia sasa jamii iwapeleke watoto
shule kuanzia elimu ya awali hadi sekondari na tuache kuwatumia watoto wadogo
kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku. Wakuu wa wilaya simamieni eneo hili la
kuondoa watoto kwenye ajira,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo pia kusisitiza viongozi wa mkoa huo
wasimamie elimu ya mtoto wa kike na kuhakikisha kuwa wanahitimu elimu ya
sekondari.
“Kuna tatizo la mimba kwa watoto wa shule. Eneo
hili pia linahitaji usimamizi ili kuwalinda watoto wa kike wamalize elimu yao. Tuwalinde
wanaposoma elimu ya msingi na sekondari, wakishafika vyuo vikuu watakuwa
wamepevuka na kuweza kufanya maamuzi ya kujilinda,” alisema.
Akihutubia kwenye mikutano ya hadhara wakati wa
ziara yake ya siku nne moani Tabora, Waziri Mkuu aliwaasa vijana wa kiume
wasithubutu kuwaoa mabinti wanaosoma, kwani kwa kufanya hivyo, wataishia
kufungwa jela miaka 30.
Pia aliwaasa wazazi wanaoamua kuwaoza mabinti zao
ili wapate mahari, nao pia wana hatari kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 endapo watabainika
kushirikiana na waoaji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 14, 2017.
No comments:
Post a Comment