Amesema licha ya
Tanzania kuwa na vivutio vingi vya utalii lakini idadi ya watalii wanaoingia
nchini kwa mwaka ni ndogo, hivyo kuna haja ya kuboresha matangazo.
Waziri
Mkuu aliyasema hayo jana (Jumatano, Agosti 23, 2017) wakati alipofanya ziara
katika mji wa kitalii wa Varadero ulioko kwenye mkoa wa Matanzas nchini Cuba.
Alisema mji wa Varadero tu unaingiza watalii zaidi ya milioni moja
kwa mwaka na unategemea kivutio kikubwa kimoja tu cha fukwe ambayo ina urefu wa
kilomita 22.
Alisema idadi hiyo ni tofauti
na Tanzania ambayo imejaliiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii huku watalii
wanaovitembelea ni wachache. “Tunatakiwa kujitangaza zaidi.”
Waziri Mkuu alitaja baadhi ya vivutio vya utalii ambavyo ni
mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, miji ya kihistoria ya Kilwa, Bagamoyo,
Stone Town pamoja na Mikindani.
“Vivutio vingine ni eneo la Oldvai George ambako binadamu wa kwanza
aliwahi kuishi, hifadhi ya Gombe ambako kuna sokwe ambao wanaishi kama
binadamu.”
Alisema Serikali itahakikisha jitihada zinafanyika katika kukuza
sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vilivyoko nchini ili
kuweza kuongeza idadi ya watalii.
Pia Waziri Mkuu aliwahamasisha Watanzania kujenga tabia ya kutembelea
vivutio vyeo vya utalii na kujifunza mambo mbalimbali na si kuwaachia wageni
pekee.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Sekta ya Utalii katika
mkoa wa Matanzas, Bw. Luis Martinez de
Armas alisema mji wa Varadero ni kivutio kikubwa cha utalii nchini Cuba.
Alisema kivutio kingine cha utalii ni hoteli zilizojengwa ndani
ya bahari, maeneo ya kihistoria na migahawa inayouza vyakula vya asili vya nchi
hiyo.
Bw. Luis alisema mwaka 1990 ndio walianza kuendeleza sekta ya
utalii katika mkoa wao na ulikuwa na hoteli 4,436 ambazo kwa sasa zimeongeza na
kufikia hoteli 20,696.
Hata hivyo Bw. Luis alisema Tanzania inavivutio vingi vya utalii
na kwamba anavutiwa na mlima Kilimanjaro pamoja na wanyama na viumbe vingine
vilivyoko katika mbuga mbalimbali. Alisema wako tayari kushirikiana na Serikali
katika kukuza sekta ya utalii.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, AGOSTI 24, 2017.
No comments:
Post a Comment