Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akitia saini kitabu cha wageni mara baada ya
kuwasili Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jijini
Dodoma kwa ajili ya kuhimiza uwajibikaji.
Baadhi ya watumishi wa Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)
(hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi
hao cha kuhimiza uwajibikaji kilichofanyika katika ofisi ya Sekretarieti hiyo
jijini Dodoma.
Kamishna wa Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mst. Mhe. Harold Nsekela
(kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kuhusu majukumu
ya ofisi yake wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na Menejimenti ya
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, alipoitembelea ofisi
hiyo kuhimiza uwajibikaji jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)
akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma (hawapo
pichani) alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi ya Sekretarieti hiyo
jijini Dodoma kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji. Kushoto ni Kamishna
wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mst. Mhe.
Harold Nsekela.
Na Mwandishi Wetu
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imetakiwa
kuwachukulia hatua kali za kinidhamu viongozi wanaokula Kiapo cha Ahadi ya
Uadilifu na kutoa Tamko la Rasilimali na Madeni lakini wanashindwa kutekeleza kiapo
hicho.
Hayo yamesemwa
na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati akizungumza na watumishi wa Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma, alipofanya ziara ya kikazi makao makuu ya ofisi
hizo jijini Dodoma yenye lengo la
kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma na kujiridhisha namna inavyotekeleza wajibu wake.
Mhe. Dkt.
Mwanjelwa amesema, baadhi ya viongozi wamekuwa wakila Kiapo cha Ahadi ya
Uadilifu na kusoma Tamko la Rasilimali na Madeni lakini maisha na tabia zao ni
tofauti kabisa na viapo wanavyoapa, hivyo ameisisitiza Sekretarieti ya Maadili kutumia
sheria kuwawajibisha viongozi wa namna hiyo kwani ni mzigo kwa taifa.
Mhe. Dkt.
Mwanjelwa amesema viapo na matamko ni lazima viendane na uhalisia, hivyo
ameitaka Sekretarieti hiyo kufanya ufuatiliaji na kuchukua hatua bila uwoga
wowote kwa kiongozi anayeenda kinyume kwani kiongozi wa namna hiyo anakosa sifa
ya kuwa kiongozi bora.
Mhe. Dkt.
Mwanjelwa amesema ni lazima kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Serikali ya
Awamu ya Tano za kupambana na viongozi ambao hawana maadili mema ili kuleta
maendeleo kwa taifa.
Aidha, Mhe.
Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa Sekretarieti hiyo kuishi na kufanya kazi
katika maadili mema ili wawe mfano kwa wanaowasimamia katika suala zima la
maadili.
“Ni lazima maadili
mema yaanzie kwetu sisi ili tunapozungumza na kutoa elimu ya maadili kwa
viongozi tuwe kioo kwani huwezi ukazungumzia maadili kwa viongozi kama wewe mwenyewe
huna maadili, hivyo ni lazima kuonyesha mfano,” Mhe. Dkt. Mwanjelwa
amesisitiza.
Awali,
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji
Mstaafu, Mhe. Harold Nsekela amesema, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma ilianzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa lengo la kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi wa umma yeyote
kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba masharti ya Sheria ya Maadili ya viongozi
wa umma yanazingatiwa ipasavyo.
Mhe. Nsekela
ameyataja majukumu ya Sekretarieti kuwa ni pamoja na kupokea matamko ya
viongozi wa umma kuhusu rasilimali na madeni yanayopaswa kutolewa kwa mujibu wa
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kuanzisha na kufanya uchunguzi wowote
kuhusu ukiukwaji wa maadili yaliyotajwa na Sheria, kupokea na kushughulikia
malalamiko na taarifa za ukiukwaji wa maadili kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma kutoka kwa wananchi na kufanya uhakiki wa Tamko la Rasilimali
na Madeni ya Viongozi wa Umma wanaotajwa na Sheria.
Mhe. Nsekela
ameyataja baadhi ya matarajio ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
kuwa ni kujenga na kuimarisha maadili ya kitaifa na kuyafanya yawe sehemu ya
jamii ili kuzuia mmomonyoko wa maadili katika nchi kwa kujumuisha somo la
maadili katika mitaala kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, kufanya
marekebisho ya Sheria zinazohusu ukuzaji wa maadili nchini ikiwemo Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na kutungwa kwa Sheria ya Kudhibiti Mgongano
wa Maslahi.
No comments:
Post a Comment