HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 04, 2019

KARIA USILINAJISI SOKA KWA MGONGO WA SIASA

NA JOHN MARWA

MBIO za sakafuni huishia ukingoni pia hakuna marefu yasiyo kuwa na ncha, hizo ni miongoni mwa methali za Kiswahili zenye mafundisho makubwa kwa kila mwenye pumzi kila iitwapo leo.

Mwanadamu aliumbwa kutumika mbele za Mwenyezi Mungu na kuwatumikia waja wake, hapa ndipo wanapatikana Mitume na viongozi katika nyanja mbalimbali.


Katika nyanja ya michezo tumekuwa na viongozi wengi wenye ueledi na utumishi uliotukuka tangu nchi hii ilipoutambua mchezo wa soka na kuufanya kuwa sehemu ya maisha ya Watanzania.

Lakini hatujawahi kuwa na kiongozi wa kariba ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Yuko tofauti kuanzia sura, mwendo, rafudhi ya kuzungumza hata fikra za kiutendaji ndani ya taasisi hiyo nyeti katika michezo nchini.

Alionekana mkombozi baada ya kuchaguliwa pale jijini Dodoma Agosti 2017, kwa kutambua umakini wake wajumbe wa Kamati Kuu walimchagua Michael Wambura kuwa Makamu wa Rais wakiamini wawili hao wataliongoza soka la Tanzania kupiga hatua.

Haikuwa hivyo, leo ni tofauti sana, Wambura hayupo tena kwenye himaya ya wajumbe wale waliomuamini na kumchagua kwa kishindo, ila Karia yupo kwa sababu ya kuwahadaa kifikra na kuwafanya kuona chaguo lao halikuwa sahihi.

Soka la Tanzania liko taabani kwa maana liko katika uangalizi maalumu japo hakuna mwangalizi ila kuna waangaliaji wa hali hiyo.

Haya yanathibitishwa na maneno ya Karia kupitia hotuba yake ya kwanza kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa TFF tangu aingie madarakani, uliofanyika juzi jijini Arusha.

Karia kwa kuthibitisha soka la Tanzania lipo kwenye chumba maalumu cha uangalizi pasipo kuwa na muangalizi kwa kuchanganya siasa na soka.

Ikiwa ligi haina udhamini, ligi haina mvuto, ligi haina ushindani wa kuanada wachezaji katika ngazi ya kimataifa yeye anafanya kazi ya kuchanganya mambo.

Katika hotuba yake moja ya vitu vilivyo leta ukakasi alijikuta akifanya kazi ya usemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jukwaa la soka

“Sisi tuko kwa ajili ya kutengeneza mpira ni vizuri tuka simama, hao Ma-Tundu-Lisu wa kwenye mpira tuwaache waendelee na U-Tundu-Lisu wao lakini sisi tutaendelea na mpira na hatutamjibu mtu yeyote tutaendelea kufanya kazi kwa utarataibu, mimi ninachowaomba tushirikiane Ofisi yangu iko wazi mimi niki wazi tunashirikiana na kila mtu ili kuendeleza mpira,” alisema Karia

Kiongozi mkubwa wa taasisi kubwa kama TFF, kusema maneno kama haya kumtaja binadamu aliyepitia mikasa mikubwa ya kushambuliwa na risasi nan watu wasiojulikana ni dhihaka kwa Watanzania na ulimwengu wa michezo kwa ujumla.

Maneno yake yanakupa ujasiri wa kusema ‘akili ndogo haiwezi kuongoza akili kubwa’ ameonyesha kutojua anaongoza tasisi ya aina gani yenye mlengo upi katika kuwatumikia wanamichezo.

Michezo Duniani kote huunganisha watu, huleta suluhisho mfano nchini Afganistan baada ya kuruhusu michezo kufanyika vitendo vingi vya kigaidi vimepungua.

Karia amekosa macho ya kuona jinsi gani viwanja vya michezo vinabeba watu wa dini zote, makabila yote, wa itikadi za kivyama aina zote bila aibu yeye anawagawanya wanamichezo amabao wana itikadi zao, makabila yao na dini zao kinyume na Sheria na kanuni za Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA).

Karia anapaswa kujitazama na kijitathimini kama bado anafa kuwa kiongozi wa michezo ambayo ni amani, upendo na urafiki ndio sehemu yake.

No comments:

Post a Comment

Pages